Home BIASHARA WAFANYABIASHARA DAR ES SALAAM WAELIMISHWA KUHUSU KODI YA ZUIO

WAFANYABIASHARA DAR ES SALAAM WAELIMISHWA KUHUSU KODI YA ZUIO

0 comment 99 views
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewaelimisha wafanyabiashara wa maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam kuhusu Kodi ya Zuio na kutoa wito kwa wamiliki wa majengo, fremu na ardhi kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi hiyo ambayo ni asilimia 10 ya kiasi cha malipo walichokubaliana katika mkataba wa upangishaji ili waiwasilishe TRA.

Akizungumza wakati wa kampeni endelevu ya elimu kwa mlipakodi ambayo kwa awamu hii itamalizika kesho jijini hapa, Afisa Msimamizi Mkuu wa Kodi kutoka Mamlaka hiyo Bw. Stephen Kauzeni alisema kuwa, kodi ya zuio inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato na inasimamiwa na TRA hivyo amewataka wapangishaji kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi hiyo wakati wanapolipwa kodi ya pango.

“Tangu tumeanza zoezi hili la elimu kwa mlipakodi tumefanikiwa kupita karibu maeneo yote ya Tabata ikiwa ni pamoja na Relini, Bima, Barakuda, Kimanga, Kisukulu na Kinyerezi. Katika maeneo yote haya tumegundua kwamba, baadhi ya wamiliki wa nyumba za biashara hawaruhusu wapangaji wao kukata kodi ya zuio ambayo inapaswa kuwasilishwa TRA kwa mujibu wa sheria.

“Tulichokifanya ni kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kodi hiyo na napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wenye nyumba na fremu mbalimbali kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia asilimia 10 ya kiasi cha malipo walichokubaliana kwenye mkataba wa upangishaji ili wapangaji hao wakiwasilishe Mamlaka ya Mapato Tanzania,” alisema Bw. Kauzeni.

Bw. Rashid Omary ni mmiliki wa fremu za biashara wa Tabata Kimanga jijini hapa ambaye amesema kuwa, amefurahishwa na elimu ya kodi ya zuio aliyoipata kutoka kwa maafisa wa TRA na amewaomba wamiliki wenzake kuhakikisha wanawaruhusu wapangaji wao kuzuia asilimia 10 ya kodi ya pango ili fedha hizo ziwasilishwe TRA kama sheria inavyoelekeza.

“Kama mimi ni mmiliki lakini nilikuwa sielewi kama wapangaji wangu wanatakiwa kunikata asilimia 10 ya kodi ya pango tuliyokubaliana kwenye mkataba ili waipeleke TRA. Hivyo elimu hii imenifungua sana na hivyo napenda kuwashauri wamiliki wenzangu wawaruhusu wapangaji wao kukata hiyo asilimia 10 kwa sababu kodi hii itarudi kwetu kupitia maendeleo yanayoletwa na Serikali katika maeneo yetu tunayoishi, alisema Bw. Omary.

Naye, mmiliki wa maduka ya Ikupa Market Bi. Hortensia Kimaro ameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania iwasajili wenye majengo ya biashara ili walipe kodi ya zuio wao wenyewe kwa sababu baadhi yao ni wagumu kuwaruhusu wapangaji wao kuzuia kodi hiyo.

Kodi ya zuio hutozwa katika maeneo tofauti ikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara, mirabaha, hisa, upangishaji na gawio mbalimbali ambapo kila eneo limepangiwa kiwango cha asilimia kinachotakiwa kulipwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter