Dar es Salaam. Takribani watu 10,000 wanatarajia kupata ajira katika kituo kikuu cha mabasi cha Mbezi Luis jijini Dar es Salaam baada ya ujenzi wake kukamilika mapema mwakani.
Akisoma ripoti ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi mbele ya Rais John Magufuli pamoja na Rais wa Malawi Lazarus Chakwera ambae yupo nchini kwa ziara ya siku tatu, waziri wa Tamisemi Suleiman Jafo amesema ajira hizo zitahusisha wafanya biashara mbalimbali, mama ntilie, bodaboda pamoja na wafanyakazi wa mabasi.
Jafo amesema ujenzi wa stendi hiyo umegharimu shilingi bilioni 70.1 ina uwezo wa kuchukua mabasi 3456 wakati inapofanya kazi na eneo la kupaki magari takribani 1,000.
Amesema kituo hicho cha mabasi kitahudumia watanzania pamoja na nchi zote jirani ikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Congo, Malawi, Zambia, Mozambique, pamoja na nchi zote za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Africa (SADC).
Waziri Jafo amesema stendi hiyo ya kisasa itakuwa ni vunja kazi kwa tanzania nzima.
“Niwaombe sana watanzania muwe mnafatilia vyombo vya habari. Mtapokuja Dar es Salaam siku zingine lazima mpate maelezo ya kutosha, kuna wengine hasa watani wangu kutoka Ruvuma na mikoa ya Kanda ya Ziwa nina wasiwasi sana wengi watakuja kupotea hapa Dar es Salaam, ” amesema waziri Jafo.
Ameeleza kuwa stendi hiyo itakapokamilika jiji la Dar es Salaam litakusanya mapato ya wastani wa shilingi bilioni 10.2 kwa mwaka.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli na mgeni wake Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi kilichopo Mbezi Luis, Dar es salaam leo Oktoba 8, 2020.