Home BIASHARA Wanawake wahamasishwa kutumia fursa za digitali kukuza uchumi

Wanawake wahamasishwa kutumia fursa za digitali kukuza uchumi

0 comment 133 views

Wanawake wa Kitanzania wametakiwa kuamka na kuwa wabunifu kwa kutumia fursa za kidigitali kukuza na kutangaza biashara zao.

Wadau wa digitali walitoa wito huo jijini Dar es Salaam wakati wa programu ya mwanamke wa wakati ujao iliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Confederation of Norwegian Enterprises.

John Ulanga ambae ni Mkurugenzi wa TradeMark Afrika Mashariki alisema kwa sasa digitali sio tena mbadala kwa kuwa ina fursa nyingi zenye matokeo chanya katika maisha ya watu.

Alisema wanawake wanaweza kuwa washindani katika kuwasilisha mada zao kwenye mitandao ya kijamii iwapo tu wataweza kufikia hadhira yao kwa maudhui sahihi na kwa muda muafaka.

“Labda kama hutaki kufanikiwa, lakini unahitaji kufikia malengo yako, ni lazima utumie fursa za kidigitali kwa sababu huko ndiko dunia ilipo na ndio njia ya kujulisha ulimwengu unachofanya,” alisema Ulanga.

Mshauri wa mawasiliano ya digitali ambae pia ni mjasiriamali Kai Mollel alisema mitandao ina fursa nyingi ambazo bado hazijatumika.

“Siku hizi wanawake wengi wanatumia muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii bila kuingiza kipato chochote, wanatumia muda wao na vifurushi vya mtandao kutafuta vitu ambavyo havina manufaa kwao, wengi hawajui fursa kubwa iliyopo katika uchumi wa digitali,” alisisitiza Mollel.

Mollel alisema bado kuna uhitaji mkubwa wa kutoa elimu na mwamko kuhusu fursa zilizopo katika masoko ya mtandaoni hususani kwa wanawake.

Anabahati Mlay ambae ni mratibu wa programu ya mwanamke wa wakati ujao kutoka ATE alisema mkutano huo wenye kauli mbiu ya “kuunganisha vipawa vya wanawake katika uchumi wa digitali” uliunganisha wanawake kutoka sekta binafsi na taasisi za uma kujadili na kubadilishana utaalamu utakaosaidia kuwawezesha wanawake kufikia ndoto zao kupitia teknolojia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter