Home BIASHARA Mkuu wa Mkoa Dar avunja mkutano wake na sekta binafsi

Mkuu wa Mkoa Dar avunja mkutano wake na sekta binafsi

0 comment 93 views

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge jana alivunja mkutano kati yake na wadau wa sekta binafsi kuhusu mazingira ya biashara na uwekezaji katika mkoa wake kutokana na kutoridhishwa na taarifa kutoka kwa watendaji wa serikali.

Watendaji hao walishindwa kutoa majibu ya matatizo sugu yaliyowasilishwa na sekta binafsi.

Uamuzi wa Kunenge ulijitokeza baada ya kusikiliza mawasilisho ya Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Wizara ya Viwanda na Biashara na kubaini kuwa hayakuwa na majibu ya changamoto za wafanyabiashara.

Mkuu wa mkoa alisema “ukweli taasisi zetu za uwakilishi tuna shida, hakuna lolote yaani sijaona kitu. Kwa hiyo naahirisha kikao mpaka siku nyingine”.

Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu ya “Mazingira Bora ya Biashara na Uwekezaji kwa Maendeleo ya Dar es Salaam, Taifa na Sekta Binafsi”, ulihudhuriwa na takribani washiriki 200, wakiwamo wafanyabiashara na watendaji kutoka taasisi mbalimbali na wizara.

Akiwasilisha mada yake, Meneja wa Kanda ya Mashariki kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC), Edward Ngezi alieleza namna kituo hicho kinavyotekeleza majukumu yake kisheria sambamba na ofisi ya taasisi zote muhimu wakati wa hatua za uwekezaji ili kuepuka usumbufu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba mwakilishi huyo alitakiwa kueleza fursa za uwekezaji na biashara pamoja na mikakati ya Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Kennedy Rwehumbira alitaja vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji ndani ya mkoa huo.

Vikwazo hivyo ni pamoja na wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga kuuza bidhaa zao kwa bei ya kuua ushindani tena mbele ya maduka ya wafanyabiashara wanaolipia kodi.

Vikwazo vingine alivyoomba kushughulikiwa ni makadirio ya kodi kuwa kubwa kuliko uhalisia wa mitaji yao huku wakidai kuumizwa na ukokotozi wa kodi unaokuwa juu zaidi ya uhalisia wa thamani ya malighafi zinazonunuliwa bila matumizi ya mashine ya EFDs.

Aliomba Serikali iwarejeshee wafanyabiashara Kodi ya Ongezeko la Thamani(VAT) inayotakiwa kurejeshwa kwao ndani ya siku 90 ya uhakiki wa serikali huku akiomba kodi ya pango kutozwa mmiliki badala ya mtumiaji wa pango ambae ni mpangaji.

Aidha, TPSF pia iliomba uongozi wa mkoa wa Dar es Salaam punguzo la tozo ya huduma kutoka asilimia 0.3 hadi asilimia 0.1 pamoja na kushughulikia changamoto ya barabara zinazokwamisha uendeshaji wa shughuli za uwekezaji.

Rwehumbira aliomba pia kushughulikia kero ya kamata kamata ya bidhaa zao barabara wanazotoa kituo kimoja kuhamishia kituo kingine.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter