Serikali ya Tanzania imetia saini mikataba sita yenye thamani ya Sh bilioni 307.9 iliyofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) kwa ajili ya kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo nishati, huduma za afya ya mimea, mazingira ya biashara na ushirikiano wa kitaalamu.
Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo leo Februari 16, jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, amesema Serikali imesaini mikataba hiyo kupitia Mpango wa Ushirikiano wa 11 chini ya Mfuko wa Maendeleo wa Ulaya (NDF).
Ameitaja miradi hiyo kuwa ni wa kuboresha sekta ya nishati wenye thamani ya Sh bilioni 96.7, mradi wa matumizi endelevu ya nishati ya kupikia wenye thamani ya Sh bilioni 82.8, mradi wa kusaidia mnyororo wa thamani katika ufugaji nyuki wenye thamani ya Sh bilioni 27.6.
Ametaja miradi mingine kuwa ni wa kuboresha huduma ya afya ya mimea nchini ili kuongeza usalama wa chakula wenye thamani ya Sh bilioni 27.6, mradi wa kusaidia kuboresha mazingira ya biashara na ukuaji wa ubunifu wenye thamani ya Sh bilioni 63na mradi wa kusaidia kuboresha mazingira ya biashara, ukuaji na ubunifu wenye thamani ya Sh bilioni 63.5.
“Kwa niaba ya serikali napenda kuushukuru sana Umoja wa Ulaya kwa misaada yake hii kwa Tanzania kwani imekuja wakati muafaka ambapo serikali inaweka mazingira wezeshi ya kukuza viwanda kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wetu,”amesema Katibu Mkuu huyo.
Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini, Manfred Fanti, amesema lengo lao ni kuhakikisha bidhaa za hapa nchini zinapata soko Ulaya huku akisisitiza umuhimu wa bidhaa hizo kuongezwa thamani.