Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza na kusema Rais Samia Suluh amedhamiria kuboresha mahusiano ya kimataifa kuchochea uwekezaji.
Waziri Mkuu amesema katika kipindi kifupi, Rais Samia ameboresha mahusiano na nchi mbalimbali ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kukuza uchumi.
Majaliwa amesema “Mh Rais amenituma niwaambie kuwa serikali anayoiongoza ipo tayari kuwapokea, kuwasikiliza na kushirikiana nanyi katika kuimarisha shughuli za uwekezaji na biashara nchini.”
Ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Agosti mwaka huu, Tanzania imeongoza kwa kuvutia kiwango kikubwa cha uwekezaji kutoka nje kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo kiwango hicho kilifika Dola za Marekani bilioni 2.9.
“Rais Samia ameongeza usimamizi wa sera za soko huria, sera za kiuchumi na kifedha zenye mwelekeo wa kuimarisha mazimgira ya biashara na uwekezaji” amesema Waziri Mkuu.
Amesema hivi karibuni serikali imeshuhudia uwekezaji kutoka kampuni mbalimbali ya Uingereza.