Home BIASHARA SABABU ZA BIASHARA NYINGI KUKOSA WATEJA.

SABABU ZA BIASHARA NYINGI KUKOSA WATEJA.

0 comment 132 views

Ni muhimu kuwa makini katika kila jambo kwa sababu maamuzi yote huwa na matokeo mbeleni. Kwa upande wa biashara, wafanyabiashara wanashauriwa kuwa makini katika kila jambo kwani wateja huwa makini na kila kitu na kutokana na mtazamo wao wanaweza kuamua kuwa wateja wa kudumu au kutafuta sehemu nyingine ya kujipatia huduma wanayohitaji.

Haya ni baadhi ya mambo yanayoweza kupelekea kupoteza wateja katika biashara

Mazoea – Ili kuwavutia wateja wengi zaidi katika biashara yako ni muhimu kuwa mbunifu na mtu ambaye haogopi kufanya mabadiliko inapobidi. Wateja wengi hawafurahishwi na wafanyabiashara wanaofanya biashara kwa mazoea. Hili ni tatizo kubwa kwa wafanyabiashara wengi na hali hii inaathiri biashara taratibu na inaweza kusababisha biashara isiendelee kwa sababu wateja wataenda kununua bidhaa kwa mfanyabiashara ambaye yuko tayari kufanya vitu tofauti na mazoea yake ya kila siku.

Muda wa kufungua – Kwa ujumla hakuna mtu anayependa kupoteza muda au kucheleweshwa. Ikiwa mfanyabiashara ana tabia ya kuchelewa kufungua biashara yake ili hali anajua kuwa mahitaji ya wateja wake huanza mapema zaidi basi ni rahisi kukosa wateja hata wale wa kudumu kwa sababu mtu akiwa na uhitaji wa huduma au bidhaa huwa anataka kuipata kwa muda muafaka hivyo ikiwa mteja anakuta pamefungwa basi atatafuta sehemu nyingine ambayo anaweza kupata huduma husika na kutengeneza mazoea ya kwenda huko kila akiwa na uhitaji.

ADVERTISEMENT

Kukosa umakini – Kuna baadhi ya wafanyabiashara si makini na biashara zao kutokana na hilo hata wateja hupungua kwa sababu mteja siku zote hufurahishwa na mtoa huduma au mfanyabiashara makini, asiye na mambo mengi na anayejua umuhimu wa huduma bora kwa mteja. Kwa mfano mfanyabiashara ambaye kila mteja akija lazima atafutwe kwa sababu anashindwa kutulia katika biashara yake, ni dhahiri wateja watachoka na kutafuta sehemu nyingine yenye bidhaa au huduma unayotoa ili waweze kuendelea na mambo mengine. Au mfanyabiashara ambaye anatumia muda mrefu kwenye simu yake badala ya kumsikiliza mteja na kuhakikisha amepata huduma anayostahili lazima akose wateja kwani tabia hii haiwafurahishi watu.

Lugha – Kama mfanyabiashara lugha yako kwa wateja inaweza kupelekea ujipatie wateja wengi zaidi au la. Kwa sababu wateja wanaokuja katika biashara yako ni wa aina mbalimbali na wanakuwa wametoka kupitia mambo mbalimbali hadi kufika katika biashara yako. Mteja ana uwezo wa kuchagua sehemu yoyote anayotaka kwa ajili ya kununua bidhaa hivyo akipokelewa na lugha mbaya ni rahisi kwake kutafuta sehemu nyingine.

Wafanyabiashara wanatakiwa kubadilika kama wanataka kupata maendeleo kwani lengo la biashara ni kukuza uchumi. Jambo la msingi la kukumbuka ni kuwa mteja ana uhuru wa kuchagua ni wapi anataka kununua huduma au bidhaa hivyo ushindani ni mkubwa sokoni na wafanyabiashara wanapaswa kubadilika ili kujenge uaminifu kwa wateja wao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter