Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Vilio vya wafanyabiashara masoko kuungua moto

Vilio vya wafanyabiashara masoko kuungua moto

0 comment 298 views

“Hapa unavyoniona vitu vyangu vyote vimeungua, nimeanzisha biashara hii kwa fedha ya mkopo na vitu vyote vimeteketea hapa, bado sijamaliza kulipa deni, sijui nafanya nini na familia yangu tunategemea hii biashara, nimebaki na deni ambalo sijui hatma yake.”

Huyu ni mmoja wa wafanyabiashara katika soko la Mbagala aliyekuwa sokoni hapo kujaribu kuokoa bidhaa zake baada ya soko hilo kuungua moto usiku wa kuamkia February 13, 2022.

Soko la Mbagala rangi tatu lililopo Wilaya ya Temeke, Dar es salaam liliungua moto.

Katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Jokate Mwegelo aliunda kamati ya kuchunguza chanzo cha moto huo.

“Tumeunda Kamati ya kuchunguza chanzo cha moto na tumeipa siku tatu hadi nne, kikubwa tumetoa maelekezo kwa Manispaa kamati ya uchunguzi ikimalizika kazi wafanyabiashara waruhusiwe kurudi sokoni kufanya biashara huku ikiwekwa mipango ya kukarabati na kuboresha soko hilo” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Alisema soko hilo lilikuwa na vizimba 388 na vibanda 20 ambavyo vimeungua, kwamba wanashukuru zimamoto waliwahi mapema na kusaidia kuokoa na walifanikiwa kutokana na miundombinu ya soko kuwa mizuri ikiwemo barabara zinazopitika.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alisema “kupitia masoko naomba wafanyabisha kwa kushirikiana na viongozi wenu kujijengea tabia ya kuimarisha ulinzi wenyewe kwani unaanzia kwenu, mimi nimechoka kusikia ajali za moto, wekeni miundombinu ya njia zinazopitika ili iwe rahisi  kukabiliana na ajali kama hizi zinapotokea.”

Akielezea tukio hilo, Katibu wa Soko la Mbagala Rangi tatu, Frank Mapolu alisema  moto huo ulianza saa 10 kasoro  huku akieleza chanzo cha moto huo bado hakijafahamika.

Alisema kulingana na maelezo ya walinzi wa soko wanasema moto ulianzia kwenye kizimba cha kuuzia dagaa na kusambaa kwa haraka kwenye maeneo mengine ya soko.

Wafanyabiashara sokoni hapo wameiomba serikali kuwasaidia katika kipindi hiki ambacho soko hilo limeungua na kuteketeza baadhi ya mali zao.

Huu ni mfululizo wa majanga ya moto katika masoko mbalimbali nchini.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Abdalla Mtinika, amekutana na wahanga wa janga la moto katika soko la Mbagala na amewataka wafanyabiashara hao kuwa na subira katika kipindi hiki ambacho wanasubiri majibu ya chanzo cha moto huo kutoka katika kamati ya uchunguzi iliyoundwa kuchunguza jambo hilo.

Mtinika pia amewataka wafanyabiashara kutojenga wenyewe soko hilo bali wasubiri maelekezo na Halmashauri itatoa fedha za kukarabati baada ya ripoti ya chanzo cha moto kujulikana na kujadiliwa katika vikao vya Halmashauri.

“Kama Uongozi wa Halmashauri tunasubiri taarifa ya uchunguzi wa Kamati ukamilike tuwaahidi tu kuwa tutafanya ujenzi wa haraka wa soko hili ili kuruhusu Wananchi kuendelea na shughuli zao za ujenzi wa Taifa”, amesema Mtinika.

 

Julai 10, 2021 soko la kimataifa la Kariakoo

Julai 10, 2021 soko la kimataifa la Kariakoo jijini Dar es salaam liliteketea kwa moto.

Katika tukio hilo, Rais Samia Suluhu Hassan aliviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliunda Kamati maalumu kwa ajili ya kuchunguza ajali ya moto huo.

Waziri Mkuu pia alitoa agizo kwa benki na taasisi za fedha kuangalia namna ya kuwaongezea muda wa kurejesha mikopo wafanyabiashara walioathirika na katika tukio hilo.

Julai 27, 2021 Majaliwa alipokea taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati CP Liberatus Sabas na kuahidi kuwa Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa.

 

Soma: Bilioni 28 kujenga Kariakoo mpya

 

Januari 16, 2022, soko la Karume

Usiku wa kuamkia Januari 16, 2022, soko la Karume lililopo Ilala jijini Dar es Salaam liliungua na kusababisha hasara ya Sh7.2 bilioni, kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi.

Ripoti ya uchunguzi ilibainisha kuwa mshumaa uliowashwa na ‘mateja’ waliokuwepo katika Soko hilo ndio chanzo cha moto mkubwa.

Akikabidhi ripoti kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mwenyekiti wa kamati ya uchunguzi, Justine Lukaza alibainisha kuwa mateja hao walikuwa wanavuta dawa za kulevya katika moja ya kibanda sokoni hapo.

 

Februari Mosi 2022, Soko la Mbuyuni

Katika tukio lingine usiku wa kuamkia Februari Mosi 2022, moto mkubwa uliteketeza sehemu ya soko la Mbuyuni lililopo katika Manispaa ya Moshi.

Mmoja wa mashuhuda aliyefika eneo la tukio alishuhudia moto mkubwa ukiwaka eneo la ndani ya soko huku gari ya Polisi ikitumika kuzima moto.

Hata hivyo, gari ya Kikosi  cha Zimamoto na Uokoaji lilifika eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji.

“Moto huu ulianza polepole majira ya saa 7:30 usiku hivyo baadhi ya wafanyabishara waliokoa mali zao, lakini kadiri muda ulivyokuwa unaongezeka ndipo ulizidi na kuwa mkubwa zaidi,” alisema mmoja wa mashuhuda.

Mashuhuda wa tukio hilo walisema hawajui chanzo cha moto huo ambao umesababisha hasara kwa baadhi ya wafanyabiashara.

Imekuwa ni sintofahamu kwa wafanyabiashara kutokana na majanga ya moto na mengine kama hayo hususani wale ambao huendesha biashara zao kwa mitaji ya kukopa ambao huishia kwenye madeni kutokana na hasara.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter