Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeelekeza watoa huduma za mawasiliano ya simu kutengeneza ‘application’ ambazo watumiaji wanaweza kufuatilia matumizi yao ya vifurushi.
Mkurugenzi Masuala ya Sekta TCRA, Dk Emmanuel Manase amesema lengo ni kupunguza malalamiko ya vifurushi kuisha kabla ya muda au bila kutumiwa.
Hayo yamesemwa Februari 22, 2022 wakati wa mkutano wa TCRA na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF).
“Ili kupunguza malalamiko, mamlaka imewaagiza watoa huduma za mawasiliano kuja na application ambayo itamwezesha mteja kufuatilia matumizi ya data katika simu yake,” amesema Manase.
“Tuna “application” mbalimbali kwenye WhatsApp zinaboreshwa mara kwa mara nazo zinatumia data. Watumiaji wengi wa simu kuna vitu vinaendelea kwenye simu yake lakini mtumiaji hajui. Uwepo wa application nyingi, nyingine hazitumii hivyo zinamaliza bundle,” amesema.
Ametaja vitu vinavyosababisha kumaliza kifurushi kwa haraka kuwa ni kuongezeka kwa kasi ya mtandao kwenye simu janja mfano kutoka 3G hadi 4G.
Pia, ubora wa video na picha unavyoongezeka maana yake matumizi nayo yanaongezeka.Ameongeza kuwa TCRA ipo katika hatua za mwisho kuwa na application yao ambayo itakuwa ikifanya kazi ya ufuatiliaji wa matumizi ya vifurushi.
“Kabla ya mwisho wa mwezi wa tatu, Mamlaka itakuja na application nyingine ambayo itawawezesha wateja kuona matumizi ya data na vifurushi, ambayo kwa sasa ipo katika majaribio,” amesema.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Jabiri Bakar amesema tafiti mbalimbali duniani zinaonyesha kuwa, gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine nchini Tanzania, zipo chini tofauti na nchi nyingine duniani, gharama za kawaida bila kujiunga na kifurushi, pamoja na gharama zilizounganishwa na kifurushi nazo zimeshuka.
Amesema Tanzania inaongoza kwa kuwa na vifurushi rahisi na salama Afrika na duniani, hivyo kila mtoa huduma ana uwezo wa kubadilisha vifurushi kila baada ya miezi mitatu (siku 90).