Mke wa Rais wa Kenya Margaret Kenyatta amewataka wawekezaji kuongeza ufadhili katika mifumo ya afya ya uzazi, vijana na watoto barani Afrika.
Akizungumza mwishoni mwa mwezi Februari, Kenyatta amesema ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi ni muhimu ili kuongeza rasilimali kusaidia sekta hiyo.
Amewaalika wafadhili kusaidia mfumo dhaifu wa uzazi na afya ya mtoto ambao amesema umelemewa na changamoto za kijamii. Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni ukeketaji, unyanyasaji wa kijinsi, mimba na ndoa za utotoni.
“Kupitia ushirikiano kati ya sekta za umma na binafsi na uwekezaji wa pamoja, tutaweza kuimarisha utendaji wetu kwenye uzazi, vijana na afya ya mtoto,” amesema Kenyatta.
Amebainisha kuwa Afrika ingeweza kumaliza vifo vya kina mama na watoto kama sekta ingekuwa na rasilimali za kutosha.
“Tunatakiwa tujiwekee uwezekano wa kuweza kufikia vifo 0 vya mama na mtoto kwa kutumia utaalamu na rasilimali muhimu,” amesema.