Home Elimu Usafi wa mazingira ni muhimu kwa malezi ya afya ya watoto

Usafi wa mazingira ni muhimu kwa malezi ya afya ya watoto

0 comment 153 views

Kipindi cha utoto wetu ndio mda wa kujifunza. Hapa ndipo akili inapevuka, tunajifunza lugha, na hata namna bora ya kutatua matatizo tunayokabiliana nayo. Katika kipindi hiki, mazingira anayokua mtoto yanaweza kuathiri sana ukuaji wa ubongo, tabia na hata ustawi wa kimwili.

Utafiti unaonyesha kwamba faida za kiuchumi kwa uwekezaji katika ukuaji wa watoto na elimu ya awali ni kubwa na zenye faida sio tu katika familia bali hata katika ngazi ya kitaifa.

“Kwa kumpa mtoto elimu inayofaa katika hatua za awali, unamtayarisha kupata maisha bora ya baadae ikiwemo ufaulu mkubwa katika elimu za ngazi za juu na hata kazi na mapato mazuri huko mbeleni,” anasema Gladys Micheal mlezi wa watoto na mfanyibiashara jijini Arusha, Tanzania.

Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika kusherehekea Siku ya Maji Duniani (Machi 22) Madam Gladys, kama wanafunzi wake wanavyomwita, alisema, hoja sio tu kumpeleka mtoto wako shuleni, lakini pia kuhakikisha kuwa shule inaweka mazingira mazuri na bora kwa malezi sahihi ya mtoto wako.

“Sio tu bora aende shule, lakini aende shule bora, yenye mazingira na malezi bora” alisisitiza.

“Ili hili lifanyike, usafi wa mazingira ni muhimu sana, hivyo leo tunapoadhimisha siku hii muhimu, ni lazima kusisitiza umuhimu wa upatikanaji wa maji safi na salama hasa katika shule zetu,” alisema mlezi huyo.

Mlezi huyo na mmiliki wa kituo cha kulelea watoto cha Joygla Early Beginner Children’s Daycare, kilichopo jijini Arusha, aliendelea kuipongeza serikali ya Tanzania kwa kuwekeza katika elimu bila malipo.

“Serikali yetu imetuwezesha kuwasomesha watoto bure, hivyo sasa ni jukumu la walezi kuhakikisha tunawapa watoto mazingira bora ya kusomea, na mazingira bora yanaanza na usafi na maji salama,” aliongezea.

Akizungumza na wageni waalikwa katika hafla hiyo, wakiwemo wawakilishi wa serikali za mtaa, wazazi na wadau wa maji na usafi wa mazingira, Bw. Richard Muluga Mwihechi ambaye ni Afisa Maendeleo Kata ya Lemara, Arusha, alitoa onyo kali kwa wazazi wasiowapeleka watoto shuleni mapema.

“Elimu sasa ni bure, hakuna tena kisingizio kwa wazazi, kila mzazi ahakikishe watoto wanaanza shule mapema,” alisema.

“Wazazi pia wana mchango mkubwa katika kuhakikisha watoto wao wanapata malezi bora mapema iwezekanavyo kwa kutenga muda wa kutafiti mazingira wanayosomea watoto,” aliongezea.

Akitaja thamani ya usafi wa mazingira na upatikanaji wa maji safi na salama kiongozi huyo alisema “hawa ni watoto, hivyo si suala la kuwasomesha darasani tu bali kuwapa huduma bora ndani na nje ya darasa… mazingira yote ya kulelea watoto wachanga lazima yawe masafi na salama na yazingatie mahitaji yao ya kimwili, kiakili na kihisia. ”

Ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Siku ya Maji Duniani, Madam Gladys alifunga hafla hiyo akisisitiza; “sisi Joygla Early Beginner Daycare tunasema kila siku ni Siku ya Maji Duniani.”

“Tunatanguliza usafi wa mazingira kuliko mengine yote. Tunahakikisha kwamba watoto wetu wananawa mikono, wana maji kwenye vyoo na pia wanakunywa maji safi na salama… hatuwezi kukadiria thamani ya maji, maji ni uhai.”

Machi 22 ni Siku ya Maji Duniani ambapo viongozi wa serikali na wamiliki wa makampuni na mashirika hukutana ili kujadili masuala ya maji duniani. Mwaka huu, Kongamano la Siku ya Maji Duniani linafanyika Dakar, mji mkuu wa Senegal.

Hili ni Kongamano la 9 la Maji Duniani likiwa na kaulimbiu ‘Usalama wa Maji kwa Amani na Maendeleo’ na linaangazia maeneo manne muhimu, usalama wa maji na usafi wa mazingira, maji kwa maendeleo ya vijijini, ushirikiano na njia za kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kama vile fedha, utawala, usimamizi na maarifa na ubunifu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter