Home Elimu Walimu watakiwa kuzingatia uwezo wa wanafunzi

Walimu watakiwa kuzingatia uwezo wa wanafunzi

0 comment 43 views

Naibu ha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka walimu wa shule za msingi na sekondari nchini kuzingatia uwezo wa wanafunzi wanapofundisha ili wanafunzi wapate elimu na ujuzi stahiki.

Hii ni kama ilivyoanishwa kwenye mtaala mpya ulioanza kutekelezwa Januari 2024 kwa madarasa ya awali, msingi na sekondari.

Dkt. Msonde ametoa wito huo kwa walimu akiwa katika shule ya Sekondari Usinge, wakati wa kikao kazi chake na baadhi ya Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Walimu waliopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora June 07, 2024.

“Mwalimu unapofundisha watoto darasa lolote hata kama umendaa mpango kazi, maazimio ya kazi na andalio la somo unapaswa kukumbuka kuwa ufundishaji wako utategemea uwezo wa watoto unaowafundisha,” Dkt. Msonde amesisitiza.

Dkt. Msonde amehimiza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inataka mabadiliko ya vitendo kwa walimu, hivyo walimu wanapaswa kuamua kuachana na mazoea ili wafundishe watoto kwa ufanisi na kwa kuzingatia weledi.

Ameongeza kuwa walimu ni lazima waamini kwamba kuna changamoto katika ufundishaji wao kwasababu haiwezekani mwalimu ufundishe watoto kiingereza mwaka mzima alafu wasijue kusoma, kuandika na kuzungumza hali inayopelekea kupata ufaulu usioridhisha katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne.

“Walimu tukiamini kwamba tuna changamoto, tuchukue hatua ya kubadilisha mitazamo yetu na kufanya tofauti na mazoea ambayo yametukwamisha na kutufikisha hapa tulipo,” amesisitiza Dkt. Msonde.

Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Mkoa wa Tabora Juma Kaponda amesema, anatamani walimu wa Kaliua na maeneo mengine nchini watekeleze hata robo ya maelekezo aliyoyatoa Dkt. Msonde ambayo yamelenga kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu kama ilivyokusudiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Msonde ameanza ziara ya kuhimiza uwajibikaji kwa walimu mkoani Tabora kwa kufanya vikao kazi viwili na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule, walimu wakuu na walimu waliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter