Na Mwandishi wetu
Kama mpango wa kutekeleza azma ya kila wilaya kuwa na zao la biashara, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida imetangaza kuwa zao la korosho litakuwa zao la kudumu na la biashara wilayani hapo ili kuongeza pato la wilaya na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo Fadhili Chimsala amesema kuwa kipato cha halmashauri kitaongezeka endapo korosho zitazalishwa kwa wingi katika eneo hilo kwani hivi sasa, halmashauri hiyo haina zao la biashara na la kudumu. Ameongeza kuwa katika msimu wa 2017/2018 malengo ya kilimo cha korosho ni kuzalisha mikorosho mipya 320,000. Kila kijiji kitapanda mikorosho 5,000 na mikorosho 30,000 itapandwa katika mamlaka ya mji mdogo wa Manyoni.
Chimsala ameweka wazi kuwa ili kutimiza malengo hayo yote, shughuli kama mikutano ya uhamasishaji, kutoa mafunzo kwa wataalamu na wakulima pamoja na uanzishaji wa vitalu lazima zifanyike. Naye Mbunge wa Manyoni Mashariki Daniel Mtuka ameshauri maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo hicho kuzingatia ushauri watakaopewa na wataalamu na wasifanye vinginevyo.