Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Mkoa wa Kagera kutenga ardhi kati ya hekari elfu 70 hadi laki moja kwa ajili ya kulima mashamba makubwa ya alizeti pamoja na michikichi.
Rais Samia amesema lengo ni kuondoa utegemezi wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Akizungumza Juni 09, 2022 wakati akiwa katika Kiwanda cha Kagera Sukari kilichopo Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera, Rais amesema
“Tumekuja na sera ya kilimo cha mashamba makubwa, moja katika mkoa tulioukusudia ni hapa Kagera, serikalini tumetenga bilioni 20 kuendeleza mashamba makubwa.
Tutapanda sunflower (alizeti) na michikichi kwa mbegu za kisasa ili tuweze kujitosheleza mafuta ndani ya nchi na ikiwezekana tupeleke nje ya nchi, lakini kwanza tujitosheleze ndani,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa “Tanzania tumekuwa tukitegemea mafuta ya kula kutoka nje lakini kutokana na janga la Uviko-19 tumepata tatizo la kukosa mafuta baada ya kufungwa mipaka hivyo hatuna budi kufanya uzalishaji wa ndani na ili tujitosheleze lazima tuwe na mashamba makubwa ya alizeti pamoja na michikichi”.