Home FEDHA Punguzo hili litapunguza mapato ya Serikali: Mwigulu

Punguzo hili litapunguza mapato ya Serikali: Mwigulu

0 comment 255 views

Serikali ya Tanzania imefuta na kupunguza tozo za miamala ya kieletroniki.

Hii imekuja baada ya kuwepo kwa mamalamiko kutoka kwa wananchi juu ya tozo hizo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ametangaza uamuzi huo Septemba 20, 2022 bungeni Dodoma.

Amesema Serikali imepunguza wigo wa tozo kuchochea matumizi ya miamala kwa ajili ya kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza tozo husika mara mbili.

“Marekebisho yaliyofanyika ni kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha ndani ya benki moja (pande zote) na kufuta tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine,” amesema.

Ameeleza kuwa wafanyabiashara (merchants) hawatahusishwa kama ilivyo kwenye kanuni za sasa.

Amesema marekebisho mengine ni kupunguza gharama za miamala kwa 10% hadi 50% kulingana na kundi la miamala.

“Ikumbukwe kuwa tozo hii ambayo viwango vyake vinapunguzwa leo hii tulikuwa tumepunguza kwa asilimia 30 kutoka kiwango cha juu iliyokuwa Sh 10,000 na kiwango hicho tena ikawa 7,000 na kiwango hicho kikapunguzwa kwa asilimia nyingine kama 60 kutoka 7,000 kwenda 4,000.

Na sasa tutapunguza kufuatana na makundi ya miamala kwa 10% hadi 50% ikiwepo miamala ya simu na sehemu ikiwepo miamala ya benki,” amesema Waziri Nchemba.

Amesema asilimia hizo zitazingatia makundi na gharama ya miamala zilizopo kwenye miamala katika makundi hayo.

Amesema marekebisho hayo yataanza kutumika Oktoba 1, 2022 ili kutoa fursa kwa mitambo kutengenezwa kwa programu hiyo mpya ambayo imetolewa.

“Naomba nisisitize ni dhahiri kwamba punguzo hili litapunguza mapato ya serikali, naelekeza fedha hizi zifidiwe kwenye kubana matumizi kwenye vyanzo vingine ndani ya serikali ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya msingi ya mafungu husika,”.

Amemwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa na maafisa masuhuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo ili miradi ya maendeleo yote isiathiriwe kwa hatua hiyo.

“Tutafute maeneo tukate kwenye chai, vitafunwa, misafara, kwenye safari za ndani na nje kwenye Wizara zetu kama Mh Rais alivyoelekeza.

Tukate mafunzo ya semina, matamasha, warsha, makundi yanayokwenda kukagua mradi ule ule wanakwenda kwa nyakati tofauti au wale wanaokwenda eneo husika kila mtu anakwenda na gari lake, ili fedha hizo ziweze kutumika kwenye maeneo mahususi maendeleo yasiathirike kwa punguzo hili,” amewasilisha waziri Nchemba.

Aidha, amesema sambamba na hatua hiyo serikali itafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji.

“Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio la pango sio ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndie anayepokea mapato kutokana na biashara au uwekezaji kwa kupangisha,”.

Amesema utaratibu huo ndio uliokuwa ukitumika kwa muda mrefu kwenye nyumba za biashara na nyumba zinazopangishwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter