Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) imeanzisha kilimo cha mkataba cha zao la ngano katika Mikoa ya Rukwa, Njombe na Makete ili kupunguza gharama ya Sh bilioni 530 kila mwaka inayotumika kuagiza ngano kutoka nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Dk. Anselm Moshi amesema kilimo hicho kinategemewa kuzalisha tani milioni 1 za ngano katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Dk. Moshi ameeleza hayo Oktoba 24, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na mwelekeo wa bajeti ya Bodi hiyo kwa mwaka wa Fedha 2022/23.
Amebainisha kuwa CPB ipo katika mkakati wa kuwawezesha wakulima wa zabibu mitambo midogo ya kukamua zabibu ili kuuza mchuzi badala ya zabibu zenyewe.
Amesema kuuza mchuzi badala ya zabibu kunaongezea thamani zao hilo ambalo limekosa wateja kwa miezi kadhaa sasa.
“Katika mpango mkakati wetu tutaingia kwenye zabibu na njia ambayo tunaifikiria ni kuwawezesha wakulima kuwa na mitambo midogo midogo ili wauze mchuzi badala ya zabibu, sasahivi hatufanyi ila kwenye mpango wetu tutafanya,” amesema Dk. Moshi.
Akieleza utekelezaji wa kazi za bodi hiyo Dk. Moshi amesema wana jukumu la kuhakikisha soko linapatikana.
Ameeleza kuwa katika mwaka 2021/22 Bodi imenunua mazao kwa wakulima tani 1978.53 yenye thamani ya Sh bilioni 69.8.
Akizungumzia changamoto amesema “tulikuwa na mzunguko mdogo sana wa biashara, tulikuwa tumeweza kufikia mzunguko (turn over) wa bilioni 15, tunashindwa kupanuka kwa sababu uwezo wa mtaji ulikuwa mdogo, lakini Rais ametuwezesha mtaji kutoka bilioni 15 mpaka bilioni 52 kwa mwaka.”