Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeanzisha mfumo rahisi wa utoaji wa risiti ujulikanao kama Visual Fiscal Devices (VFD) ili kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara anapata mashine ya kutolea Risiti za Kielektroniki (EFD) kwa njia rahisi na isiyo na gharama.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ameeleza Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Subira Khamis Mgalu aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kugawa mashine za kutolea risiti EFD kwa wafanyabiashara ili kuongeza wigo wa walipa kodi.
Chande alisema kuwa mfumo huu wa kisasa wa utoaji wa risiti hauhitaji kutumia mashine kama ilivyo sasa badala yake mtumiaji anaweza kutumia vifaa vingine vya kieletroniki kama vile simu janja, kompyuta na vishikwambi kutoa risiti zilizounganishwa na mfumo wa TRA.
“Mfumo unaendelea kutumika na kusambaa nchi nzima na hauna gharama badala yake mtumiaji ataingia gharama ndogo ya bando ili kupata mtandao wakati wa matumizi”, alifafanua naibi Waziri.
Aidha, alisema kuwa wafanyabiashara wanaruhusiwa kisheria kujirejeshea gharama ya ununuzi wa mashine za EFD wakati wa uandaaji wa hesabu zao za kodi wanazopaswa kulipa.
128