Home KILIMO Wadau zao la muhogo watakiwa kuongeza nguvu kwenye uchakataji

Wadau zao la muhogo watakiwa kuongeza nguvu kwenye uchakataji

0 comment 105 views

Wadau wa zao la muhugo nchini wametakiwa kushikamana na kuongeza nguvu katika uwekezaji wa viwanda na mashine za uchakataji wa zao la muhogo.

Hiyo itawawezesha kulifikia soko la Ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa Tanzania ina nafasi ya kuzalisha bidhaa za muhogo na kuuza katika soko lenye watumiaji zaidi ya milioni 472.5.

Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade Latifa Khamis ameeleza wakati akifungua kongamano la biashara la wadau wa muhogo Tanzania lilofanyika sambamba na mkutano mkuu wa tatu wa Wazalishaji na Wasindikaji wa Muhogo Tanzania (TACAPPA) unaofanyika kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwl. J. K Nyerere jijini Dar es Salaam.
Amesema takwimu za sasa zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2017 na 2021 wastani wa kiasi cha tani 49,555 za bidhaa za muhogo zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 9.19 ziliuzwa katika soko la kikanda la Afrika Mashariki.

Hata hivyo amesema Tanzania imeingiza bidhaa za muhogo hususani wanga na unga ambapo mwaka 2021 iliingiza takribani tani 17.68 zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 4.72 sawa na Shilingi bilioni 10.88.
“Uzalishaji wa zao hili unaendelea kuimarika, hivyo tunaweza kupunguza kuagiza kiasi hicho cha wanga na endapo tutaongeza uchakataji wa mazao ya muhogo hapa nchini badala ya kuagiza kutoka nchi za India, China, Pakistani na Uturuki,” amesema.
Ameitaja Congo kuwa nchi yenye fursa kubwa ikiwa na watu milioni 95 ambapo asilimia 70 ya wakazi wake wanatumia bidhaa za muhogo kwa ajili ya chakula ambazo huzipata ndani ya nchi na nyingine kutoka nchi jirani ikiwemo Tanzania.

“Fursa ya soko ipo kwa Ukanda wote wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati ambapo nchi za Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda ni wanunuzi wakuu wa bidhaa za muhogo kutoka Tanzania,” ameeleza Khamis.

Kongamano hilo lina kauli mbiu inayosema ‘Ongeza tija, panua fursa za masoko muhogo unalipa’.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter