Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) José Graziano de Silva anategemewa kuanza ziara ya siku tano hapa nchini kuanzia kesho, ambapo atapata fursa ya kufanya mikutano na mazungumzo na maofisa waandamizi kutoka serikalini pamoja na wadau mbalimbali kutoka sekta zisizo za kiserikali.
Mkurugenzi huyo pia anatarajia kukutana na Rais John Pombe Magufuli pamoja na Rais Mohamed Shein wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Taarifa kutoka Ofisi ya Mawasiliano ya FAO nchini inasema kuwa Graziano de Silva atafanya mikutano na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Charles Tizeba pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Zanzibar Hamad Rashid Mohamed.
Ziara hiyo ni katika maadhimisho ya miaka 40 ya FAO hapa nchini na Mkurugenzi huyo atakutana na uongozi pamoja na wafanyakazi wa FAO hapa nchini na baadaye kuhudhuria hafla maalum ambayo itahudhuriwa pia na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ili kusherekea maadhimisho hayo.