Home MAHOJIANO Bata wawili hadi kumiliki bata 1,000

Bata wawili hadi kumiliki bata 1,000

0 comment 176 views

Sio lazima uingie darasani na upate elimu katika mfumo rasmi ndipo uweze kufanikiwa katika maisha. Ndivyo wanavyoweza kusema kikundi cha Maisha Mazuri kilichopo Pugu, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

“Tulipata mafunzo ya uzalishaji kanisani tukiwa katika ibada, kijana mwenzetu akasema yeye ana bata, tukaanzisha kikundi tukiwa wanachama sita, akatupatia bata wawili jike na dume tukaanza kuwafuga,” anaeleza Kibali Shauri, Mwenyeketi wa Kikundi cha Maisha Mazuri.

Anasema kikundi hicho kilichoanzishwa mwaka 2019 na wakianza kwa kufuga bata wawili, ilipofika mwaka 2021 walikuwa na jumla ya bata 1,000.

“Baada ya kuona mradi wetu wa bata unaendelea vizuri tuliamua kufikiria kuanzisha kitu kingine ambapo tuliuza bata 500 na tukaweza kununua kiwanja chetu eneo la Chanika, kata ya Buyuni.

Tuliuza bata kwa watu mbalimbali na bei ya bata hutegemea na ukubwa kwa wastani ni kuanzia Sh 25,000 hadi Sh. 30,000.

Tulianza kutengeneza vikoi na sabuni za maji. Mtaji wetu wa vikoi kwa sasa ni Shilingi laki tatu na tulianza na mtaji wa Shilingi laki moja,” amesema Shauri.

Shauri anaeleza kuwa kupitia miradi yao hiyo wanategemea kununua mashine ya kusaga na kukoboa nafaka ili waweze kuendesha miradi hiyo ikiwemo ufugaji wa bata.

“Katika ufugaji bata wanakula sana, yani wanakula muda wote na kwa siku tunanunua pumba na hawa bata wanakula gunia moja la pumba kwa siku. Sasa tukiwa na mashine chakula cha bata tutakipata kwa urahisi tofauti na sasa ambapo tunatumia gharama kubwa kununua vyakula.

Tuliendelea kuuza bata ambapo kwa sasa tumebaki na bata 100 kwa ajili ya mbegu, wanaendelea kuongezeka” anaeleza Shauri huku na kusema bata hutumia siku arobaini kuatamia mayai hadi kutotoa vifaranga.

Akielezea changamoto katika biashara ya sabuni anasema wazalishaji wa sabuni ni wengi huku wengi wao wanatengeneza sabuni zisizo na viwango na kuharibu soko la bidhaa hiyo.

“Sisi bado ni wajasiriamali wadogo, tunajitahidi sana kutengeneza sabuni zetu katika kiwango lakini kutokana na baadhi ya wajasiriamali kutengeneza bidhaa zisizo na viwango wote tunaonekana sawa,” amesema.

Amewataka wajasiriamali nchinu hususani wadogo kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa zao ili kukuza soko na kuaminika na wateja wao.

Kikundi hicho pia kimeishukuru Halmashauri ya jiji la Ilala kwa kuwaunganisha katika maonesho mbalimbali ya bidhaa ambapo wanapata fursa ya kujifunza na kuonesha bidhaa zao.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter