Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Bila mikopo, wajasiriamali wajiajiri vipi?

Bila mikopo, wajasiriamali wajiajiri vipi?

0 comment 62 views

Vijana wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wanapiga hatua katika maisha kwa namna moja ama nyingine ili kujikwamua na hali ngumu. Katika miaka ya hivi karibuni, watu wa rika hili wamekuwa wakijiingiza katika shughuli za kilimo, ufugaji pamoja na ujasiriamali. Licha ya jitihada zote za vijana kujikomboa kiuchumi, mikopo kutoka taasisi mbalimbali za kifedha bado inabaki kuwa changamoto kubwa inayowakabili. Wengi wanashindwa kwenda mbali zaidi kimaendeleo kutokana na ukosefu wa mitaji ya kutosha.

Ili wazo la biashara lisibaki kuwa wazo tu, ni lazima mjasiriamali apatiwe mkopo ili afanyie utekelezaji wazo lake na lipate kumlipa na kumuingizia faida. Bila ya kufanya hivyo vijana wengi wataendelea kuwa nyuma kimaendeleo sababu tu wanashindwa kutoka hatua moja kwenda nyingine kwa kukosa mitaji.

Taasisi za kifedha zimekuwa kikwazo kwa vijana wengi kujiendeleza kutokana na masharti magumu wanayoweka hivyo wengi kushindwa kuyatimiza, hali inayopelekea wao kukosa mikopo hiyo kwa ajili ya biashara zao. Kwa vijana wengi wanaojikita na ujasiriamali kumiliki mali isiyohamishika, kuwa na kumbukumbu za taarifa rasmi, wadhamini na hata mali ambazo zinahamishika bado ni vigumu kwa kuwa ndio kwanza wanaanza hivyo wanakosa yote hayo.

Inaeleweka kuwa taasisi hizi za kifedha pia zinafanya biashara hivyo ni lazima kuwepo na vigezo na masharti fulani katika utoaji huduma zao. Lakini kwanini kusiwe na mazingira rafiki kidogo kwa ajili ya upatikanaji wa mikopo hii? Hali ilivyo hivi sasa, wengi wanakatishwa tamaa kutokana na ugumu uliopo katika upatikanaji wa mikopo hivyo mawazo yao hubaki kuwa mawazo tu na ndoto zao za kujiajiri huishia hapo.

Ni muhimu kuwa na suluhisho mbadala ambalo litapelekea vijana wengi zaidi kuweza kupatiwa mikopo hii ili kutimiza malengo yao kimaisha. Lengo letu sote ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua mbele kimaendeleo hivyo kwanini upatikanaji wa mikopo uturudishe nyuma? Bila ya vijana kupata mikopo hii, hawawezi kuanzisha biashara ambazo zinaweza kuzalisha ajira mbalimbali kwa vijana wengine katika jamii. Na bila ya biashara hizi kusimama serikali nayo inakosa mapato hivyo changamoto hii walionayo wajasiriamali inaathiri jamii nzima kwa kiasi fulani.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter