Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta zinazoanza Machi 1, 2023 ambapo mafuta ya taa yamepanda kwa wastani wa Shilingi 39 kwa mikoa ya Mtwara, Dar es Salaam na Tanga.
Taarifa hiyo inaonyesha kuishiwa kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Tanga hivyo kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.
“Kutokana na kuisha kwa mafuta ya taa kwenye matanki ya kuhifadhia yaliyopo Tanga, waendeshaji wa vituo vya mafuta kwenye mikoa ya Kaskazini wanashauriwa kuchukua mafuta ya taa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam,” imesema taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa (Ewura), Dk James Mwainyekule.
Taarifa hiyo pia imeonyesha katika bandari tatu za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga zinazopokea mafuta ni mbili pekee (Tanga na Dar es Salaam) ndio zenye matanki ya kuhifadhia mafuta ya taa.
Kutokana na kuisha kwa mafuta ya Tanga katika Bandari ya Tanga, hivyo nchi nzima kwa sasa inategemea mafuta ya taa kutoka Bandari ya Dar es Salaam huku athari ya kuongezeka kwa bei ya mafuta hayo imeongezeka.
“Bei ya mafuta ya taa mkoani Tanga imeongezeka kutoka Sh 3,107 Februari Hadi Sh 3,144 Machi, huku Mtwara ikiongezeka kutoka Sh 3,134 hadi Sh 3,170 mwezi huu,” imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inasema bei za rejareja za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam yamepanda kwa Sh 149/lita, Sh 25/lita na Sh 37/lita, mtawalia ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita (Februari 1, 2023).
Kwa Mikoa ya Kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara), bei za rejareja za Machi 2023 kwa mafuta ya petroli na dizeli yanapungua kwa shilingi 64 kwa lita na shilingi 209 kwa lita, mtawalia, ikilinganishwa na toleo la tarehe 1 Februari 2023.
“Kwa mikoa ya Kusini (Mtwara, Lindi na Ruvuma) bei za rejareja za Machi kwa petroli zinaongezeka kwa Sh 138kwa lita wakati mafuta ya dizeli inapungua kwa Sh 68kwa lita”, inaonyesha taarifa ya Ewura.