Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa, Adolf Mkenda amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) Nathan Belete Jijini Dodoma Machi 23, 2023 na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu sekta ya elimu.
Waziri Mkenda, ameishukuru (WB) kwa kuendelea kusaidia sekta ya elimu.
Ameeleza kuwa, kwa sasa wizara ipo katika kufanya mageuzi makubwa ya kielimu kwa kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya Mitaala ili kuwezesha kutoa elimu ujuzi.
Prof. Mkenda amesema serikali inaendelea kuwekeza katika sekta elimu kwa kuwa inatambua uwekezaji katika sekta hiyo utaendelea kunufaisha vizazi hadi vizazi, na kuongeza kuwa mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika yanahitaji uwekezaji wa kutosha.
“Mabadiliko haya yanalenga kuwawezesha vijana kuweza kuyamudu mazingira yanayowazunguka pamoja na kuwa na ujuzi utakaowasaidia kujiajiri ama kuajiriwa,” ameeleza Waziri.
Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Carolyne Nombo ameishukuru WB kwa kuendelea kufadhili miradi katika sekta ya elimu ambapo ameitaja baadhi ya miradi kuwa ni BOOST, HEET, ESPJ na SEQUIP ambayo imesaidia kwa kiwango kikubwa katika kuboresha sekta ya elimu.
Vilevile, ameshukuru kwa utayari wao wa kufadhili mradi wa ESPJ awamu ya pili kwani utasaidia Wizara kutekeleza mpango wake wa kuviwezesha vyuo Maendeleo ya Wananchi kuwa na mafunzo ya muda mrefu.
Akielezea utekelezaji wa Mradi wa HEET, Katibu Mkuu huyo amesema Wizara imejipanga kuutekeleza kwa ufanisi hasa katika ujenzi wa kampasi 14 katika mikoa isiyokuwa na Taasisi za elimu ya juu na kumhakikishia kwamba Wizara ina nguvu kazi ya kutosha na yenye uwezo wa kutekeleza miradi hiyo kwa kasi ili kufikia malengo kwa haraka zaidi.
Mkurugenzi Mkazi Nathan Belete ameipongeza Wizara kwa kutekeleza miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa ufanisi na kuahidi kuendelea kufadhili miradi hiyo ikiwemo mageuzi makubwa yanayotaraajiwa kufanyika katika sekta ya elimu nchini.