Home Elimu 10m kwa mshindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwl Nyerere

10m kwa mshindi wa Tuzo ya Taifa ya Mwl Nyerere

0 comment 138 views

Kilele cha Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kinatarajia kufanyika Aprili 13, 2023 Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na waandishi mahiri kutoka nchi mbalimbali duniani.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda, amesema hayo Machi 29, 2023 kisiwani Zanzibar wakati wa mkutano na waandishi wa habari.

Ameeleza kuwa tuzo hizo zitakuwa zikifanyika kila mwaka tarehe 13 Aprili ikiwa ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Waziri Mkenda ametaja malengo makuu ya tuzo hizo kuwa ni kukuza uandishi bunifu, kukuza usomaji, kuimarisha sekta ya uchapishaji na uhifadhi na kueneza utamaduni wa nchi yetu

“Serikali inatamani wapatikane waandishi mahiri wa Kitanzania ambao uandishi wao utashindanishwa katika tuzo za kimataifa.

Tungependa huko mbele ya safari tuwe na waandishi bunifu wa Kitanzania ambao uandishi wao utakuwa maarufu sana duniani, watu watatafsiri vitabu vyao katika lugha mbalimbali ili nao waweze kushinda tuzo za kimataifa kama ya Nobel,” amesema Prof. Mkenda

Ameeleza kuwa tuzo hii itatolewa kwa wanaoandika kwa lugha ya Kiswahili na itakuwa inatolewa katika nyanja sita ambazo ni riwaya, hadithi fupifupi, mashairi, vitabu vya watoto, tamthilia na tafsiri ya vitabu vingine ambapo kwa mwaka huu tuzo zitatolewa katika uandishi wa Riwaya na Mashairi.

“Katika kila nyanja mshindi wa kwanza atapewa kitita cha Shilingi milioni 10, wa pili milioni 7 na wa tatu milioni 5. Wengine 7 wataungana na hawa watatu jumla 10, kila mmoja atapewa cheti cha kutambuliwa,” amefafanua Waziri Mkenda.
Ali Abdulgulam Hussein, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar amesema mkutano na wanahabari umefanyika Zanzibar kwa kuwa tuzo hizo zinahusisha pande zote mbili za muungano.

“Mkutano huu kufanyika huku Zanzibar ni kuonesha kuwa hizi Wizara zetu mbili zinafanya kazi kwa ushirikiano na hili suala linahusu waandishi bunifu kutoka pande zote mbili,” amesema Ali Hussein.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter