Home VIWANDAMIUNDOMBINU Upanuzi bandari ya Mtwara kupunguza gharama za usafirishaji

Upanuzi bandari ya Mtwara kupunguza gharama za usafirishaji

0 comment 136 views

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amesema upanuzi wa bandari ya Mtwara kwa kiasi kikubwa utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mafuta na kusaidia malighafi hiyo kushuka moja kwa moja mkoani Mtwara tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo ni lazima yashushwe jijini Dar es salaam kisha kusafirishwa tena hadi mkoani humo. Rais Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na washiriki wa kongamano la kujadili hali ya siasa na uchumi wa nchi lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) ambapo ameeleza kuwa, bandari ya Mtwara itakuwa kituo cha biashara kwa mikoa ya kusini pamoja na nchi za jirani.

“Hatuwezi kusafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara karibu kilometa 540 wakati tunaweza kushushia huko huko na tukayasambaza lakini pia tumeamua kuipanua bandari ya Tanga nayo lazima tuipanue kwa sababu kuna kiwanda kinajengwa cha kuzalisha saruji ambayo itauzwa ndani na nje ya nchi. Tumeamua kuunganisha nchi jirani za Rwanda na Burundi kwa reli ya kisasa ya ili wanapotumia bandari ya Dar kwa ajili ya kusafirisha bidhaa wapate urahisi na  hii itaiongezea nchi yetu pato kwa kukusanya kodi. Huwezi kuongelea kukua kwa uchumi kama hauna umeme wa uhakika na wa bei nafuu tukasema lazima tuwe na umeme wetu na ndiyo maana tukaanza na mradi wa SGR kwa sababu ni umeme wa maji na utakapoanza bei  ya umeme itashuka”. Ameeleza kwa undani Rais Magufuli.

Mbali na hayo, Rais Magufuli amezungumzia ndege binafsi ya DreamLiner na kusema uwepo wa ndege hiyo utasaidia kukuza sekta ya utalii kwani watalii kutoka mataifa mbalimbali sasa watapata nafasi ya kuja nchini.

“Watalii walikuwa hawaji nchini kwetu kwa sababu hatukuwa na ndege yetu binafsi, huwezi kutumia shirika la ndege la jirani ili kuleta watalii nchini kwako ndiyo maana sisi tukaamua kununua ndege zetu wenyewe na kufufua shirika letu la ndege na lengo kubwa ni kuinua sekta ya utalii”. Amesema Rais Magufuli.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter