Home VIWANDAUZALISHAJI Msitoroshe madini: Rais Samia

Msitoroshe madini: Rais Samia

0 comment 127 views

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wachimbaji wadogo wawe wazalendo kwa kuacha kutorosha madini.

Rais Samia amesema hayo wakati wa utiaji saini kati ya serikali na kampuni tatu za madini kutoka Australia Chamwino Dodoma April 17, 2023.

“Niwaombe sana wachimbaji wadogo sasa ule utoroshaji hebu tuwe wazalendo zaidi. Tuna viwanda ndani vya kuchakata madini, na viwanda hivi vinalalamika havina malighafi ya kutosha, niombe sana Waziri na wachimbaji wadogo tujidhatiti kulinda madini yetu ili viwanda hivi viende vikapate malighafi ya kutosha,” amesema Rais Samia.

Amesema katika hatua ya kunyanyua sekta ya wachimbaji wadogo serikali ilisaini mikataba ya kupeleka nishati ya umeme katika maeneo ya wachimbaji wadogo na kuwafanya wachimbe zaidi kwa utaalamu na teknolojia mpya.

Akizungumzia mikataba iliyosainiwa Rais amesema “kama mnavyofahamu nchi yetu imebarikiwa madini adhimu duniani kama graphite au kinywe, na mengine ya kipekee kwa uadimu na yaliyo nadra kupatikana.

Madini haya yanapatikana katika maeneo mbalimbali ya nchi kulingana na ukanda wa kijiolojia uliopo katika maeneo hayo.

Kuna maeneo ambayo zamani tulikuwa tunaamini ni maskini sana, hayana rutuba hayana vyanzo vingine vya fedha, kumbe Mungu ameficha mali huko chini, mali ambayo sasa tumejua ni mali na maeneo yale sasa yanakwenda kunyanyuka.”

Ameitaja mikoa ya Lindi na Morogoro kuwa mikoa iliyopo katika ukanda wa madini kinywe (Graphite) na mkoa wa Songwe upo katika ukanda wenye madini adimu (rare earth element).

Ameeleza kuwa utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulianza mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbali.

Amesema kutokana na utafiti huo hadi sasa kuna kiasi cha machapo tani milioni 67 zenye wastani wa 5.4% ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika eneo la kijiji cha Chilalo ambayo yatachimbwa kwa muda wa miaka zaidi ya 18.

Tani milioni 63 zenye wastani wa 7.6% ya madini ya kinywe yamegundulika katika eneo la kijiji cha Epanko ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18.

Tani milioni 18.5 zenye 4.8% ya madini adimu yamegundulika katika kijiji cha Ngwala- Songwe ambayo yatachimbwa kwa muda wa miaka 20.

“Madini haya ya kinywe na adimu yapo katika orodha ya madini ambayo kwa sasa yanajulikana kama madini muhimu ya kimkakati duniani.

Hii ni kwasababu yanahitajika sana katika teknolojia mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo hutumika kutengenezea betri za magari ya umeme, vifaa vya kieletroniki na mitambo mbalimbali,” amesema Rais.

Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na madini hayo muhimu na ya kimkakati kwa maendeleo ya dunia katika karne hii.

“Hii imeifanya nchi yetu kuangaliwa au kutamaniwa na wawekezaji wakubwa duniani,” amesema Rais Samia.

Amesema katika siku zijazo Tanzania itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini hayo na kuvutia uwekezaji mahiri.

Amesema ni matumaini yake sekta ya madini itazidi kukua na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Aidha, Rais Samia amekubali kuwa mgeni rasmi katika shughuli ya wanawake wachimbaji madini hapo mwakani.

“Nimepokea ombi la kuwa mgeni rasmi katika shughuli ya wanawake wachimbaji madini, ombi limekubaliwa,” amesema Rais Samia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter