Home BIASHARAUWEKEZAJI Tanzania yaishukuru Taasisi ya mikopo ya UK

Tanzania yaishukuru Taasisi ya mikopo ya UK

0 comment 121 views

Serikali imeishukuru Taasisi ya Uingereza inayohusika na utoaji mikopo ya UK Export Finance (UKEF), kwa kukamilisha mchakato wa utoaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi kadhaa ya maendeleo nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba na ujenzi wa miundombinu ya barabara visiwani humo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa shukrani hizo jijini Dodoma, akifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi.

Dkt. Nchemba ameiomba taasisi hiyo, kuangalia uwezekano wa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tano na sita cha reli ya kisasa kinachoanzia Isaka hadi Mwanza chenye urefu wa kilometa 249 na mradi wa maji wa Bwawa la Farkwa kwa ajili ya kuondoa changamoto ya uhaba wa maji katika Jiji la Dodoma.

Amesema kuwa mradi wa reli ya kisasa unaombewa ufadhili wa kipande cha Isaka hadi Mwanza ambao taratibu zake za ununuzi zimekamilika na mkandarasi amepatikana pamoja na kipande cha reli cha kuanzia Kaliua hadi Kalemi kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo ambao uko katika hatua za ununuzi.

Ameeleza kuwa mradi huo utafungua biashara katika ukanda huo na kuchochea uchumi na maendeleo ya watu.

Pia, ameiomba Taasisi hiyo kuitafutia Tanzania wawekezaji watakao wekeza katika miradi mbalimbali ya uzalishaji ukiwemo mradi wa barabara ya kulipia ya Chalinze hadi Morogoro ambayo baadae imekusudiwa kufika hadi Dodoma.

“Miradi hiyo ni mkakati wa Serikali, ikiongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wenye lengo la kukuza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi,” amesewa Nchemba.

Mkurugenzi Mtendaji wa UK Export Finance (UKEF), Tim Reid, ameihakikishia Tanzania kupata fedha kwa ajili ya miradi hiyo lakini pia kuendelea kufadhili miradi mingine ya kimkakati itakayowasilishwa na Serikali ikiwemo maji na nishati.

Amesema Taasisi hiyo imekamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Pemba pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara Visiwani Zanzibar na kwamba fedha hizo zitatolewa mara tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya kimkataba.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter