Home KILIMO Serikali kusajili wakulima

Serikali kusajili wakulima

0 comment 118 views

Katika kuboresha kilimo nchini, serikali imesema itafanya usajili wa wakulima ili kujua idadi gani ya watu wanajishughulisha kwenye kilimo.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hayo wakati akihutubia katika tamasha la utamaduni lililofanyika Bulabo mkoani Mwanza.

“Tunakwenda kuweka jitihada mbalimbali ili tukuze kilimo chetu. Cha kwanza tunachokifanya na ninaomba wakulima mnisikilize vizuri ni usajili wa wakulima wetu.

Kazi hiyo imeanza katika maeneo mbalimbali, tulianza wakati tumeanza na ruzuku ya mbolea, kusajili wakulima, na tutaendelea kusajili ili tujipange zaidi kwa huduma zao kwa upande huo.”

Amesema mkakati mwingine ni kuongeza thamani ya mazao na kuvutia sekta binafsi kuweke viwanda vya mazao.

Aidha, Rais Samia amebainisha kuwa akiba ya chakula kwa sasa nchini ni takribani tani laki mbili na hamsini.

“Kwa kuanzia, mwaka huu mavuno haya yaliyoanza, tunakwenda kumwaga fedha kununua chakula tunataka kuwa na hifadhi ya tani laki tano kwa mwaka huu tunaoanzia.

“Nchi yetu iwe na tani laki tano, na hii ni tani tutakazohifadhi kwenye maghala yetu. Nimeshampa kibali Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha atoe fedha tuanze kununua mazao sasa. Niwaombe sana wakulima mazao tusivushe kutoa njee, tusubiri Wizara inakuja kununua mazao.”

Ameziomba familia zote za wakulima nchini kuweka chakula cha kutosha kwa ajili yao.

“Sisi kwenye serikali huwa tunapiga mahesabu ya akiba ya chakula, kwa nchi yetu hapa, hesabu ya akiba iliyopo kwenye maghala ya serikali, tani moja itahudumia watu mia moja themanini, hesabu hii haikubaliki kabisa, tunataka turudi tuwe na akiba ambayo tani moja itahudumia watu ishirini.”

Amewataka wakulima kutunza na kuweka akiba ya chakula cha kutosha.

Aidha Rais Samia ametumia tamasha hilo kuwaomba machief wenzake kusimamia vijana na kuwalea katika maadili ya Taifa.

“Katika sensa yetu ya mwaka jana tunaambiwa kuwa vijana ndio kundi kubwa sana la watu waliopo Tanzania. Vijana hwa wanataka kulelewa, kuelekezwa, vijana wanataka kuoneshwa njia.

Tukiwaacha waende wanavyokwenda na usasa, Taifa limeharibikiwa. Walezi wa vijana hawa ni sisi viongozi wa kijadi, machief, wazazi na viongozi wa serikali. Vijana hawa bila usimamizi taifa linapotea linakwenda hovyo na watatuharibia taifa letu” amesema Rais Samia.

Tamasha hilo limebeba kauli mbiu isemayo “Mtanzania na Maendeleo”.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter