Home VIWANDANISHATI Bei ya petroli, dizeli yashuka

Bei ya petroli, dizeli yashuka

0 comment 93 views

Bei ya mafuta ya Petroli na dizeli imeshuka kwa mwezi Julai katika mikoa inayochukua mafuta katika bandari ya Dar es Salaam na Tanga.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) inaonyesha kuwa ya petroli kuanzia Julai 5, 2023 imeshuka kwa Sh137 na dizeli kwa Sh 118 ikilinganishwa na mwezi Juni.

Hiyo inafanya bei ya petroli kuwa Sh 2,736 na dizeli kuwa Sh 2,544 kwa lita.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa, bei ya mafuta ya taa kwa Julai 2023 itaendelea kuwa ile iliyotangazwa mwezi Juni (2,698 bei kikomo za jumla) kwa kuwa hakuna shehena iliyopokelewa mwezi Juni.

“Kwa mikoa ya kaskazini (Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara) bei hiyo ya rejareja kwa mafuta ya petroli imeshuka kwa Sh188 kwa lita na kuwa Sh2,724 huku dizeli ikishuka kwa Sh 58 kwa lita na kuwa Sh 2,760,” inaeleza taarifa hiyo.

Huku bei ikiendelea kusalia kwa mikoa ya kusini na ile inayochukua mafuta yake katika bandari ya Mtwara.

“Hakuna shehena ya bidhaa za mafuta iliyopokelewa kupitia Bandari ya Mtwara kwa Juni 2023. Hivyo basi, bei ya rejareja ya dizeli kwa mwezi Julai 2023 itaendelea kuwa ni ile iliyotangazwa katika toleo la tarehe 7 Juni 2023,” imesema taarifa hiyo.

Hata hivyo taarifa ya EWURA inafafanua kuwa kutokana na upungufu wa bidhaa ya petroli katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Mtwara, waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa ya Kusini wanashauriwa kuchukua mafuta hayo katika bandari ya Dar es Salaam.

“Bei za rejareja za mafuta katika mikoa hiyo zitazingatia bei kikomo ya rejareja ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika.”

Taarifa hiyo imebainisha kuwa tofauti ya bei kutoka sehemu moja kwenda nyingine inatokana na tofauti ya bei ya mafuta katika bandari ambayo mafuta yamepakuliwa na gharama za usafirishaji.

EWURA imeeleza kuwa mabadiliko hayo yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia, gharama za uagizaji (BPS Premium) na thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter