Home VIWANDAUZALISHAJI Uwindaji wa kitalii unachangia bilioni 30

Uwindaji wa kitalii unachangia bilioni 30

0 comment 82 views

Serikali inakusanya takriban Shilingi Bilioni 30 kwa mwaka kutokana na Uwindaji wa kitalii nchini.

Uwindaji huo ambao unachangia katika Pato la Taifa hususani fedha za kigeni, pia unachangia ajira rasmi na zisizo rasmi kwa jamii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ameeleza hayo wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii nchini Julai 11, 2023 jijini Arusha.

Waziri Mchengerwa amesema kiasi hicho ni kidogo ukilinganisha na utajiri wa rasilimali za wanyamapori hapa nchini ambapo ameitaka kamati hiyo kufanya kazi na kujiwekea malengo makubwa zaidi.

Aidha, ameitaka kamati hiyo kuzitambua changamoto zinazokabili tasnia hiyo ili kuja na mikakati ambayo itasaidia kuboresha sekta hiyo.

Katika hotuba yake Mchengerwa amesema ameiunda kamati hiyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa kifungu cha 38 (1) na (2) ya Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori sura ya 283.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya Sera na Sheria za Mataifa yanayoleta watalii wengi wa uwindaji, mabadiliko ya tabia nchi, uvamizi wa mifugo katika vitalu vya uwindaji wa kitali.

Aidha, ametaka ugawaji ufanyike kwa uwazi ili kuendana na wakati wa sasa na kufanya tasnia hiyo ichangie kwa kiwango stahiki kwenye uchumi wa taifa huku akitaka kasoro zote zilizojitokeza siku za nyuma zirekebishwe.

“Kamati hii inatakiwa kuboresha changamoto zote ili tasnia ijiendeshe kibiashara na kupunguza urasimu na mikinzano isiyokuwa na tija kwa Taifa.

Ni imani yangu kwamba, kwa kuzingatia ushauri utakaotolewa na kamati hii tasnia ya Uwindaji wa Kitalii itazidi kuimarika na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” amesema.

Ameeleza kuwa, kamati itasaidia kuhakikisha vitalu vyote vinapata wawekezaji ili kuongezea mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na vitalu 43 ambavyo kwa sasa vipo wazi.

Aidha, amesema anatarajia kamati hiyo itafanya kazi kwa ufanisi na weledi katika utendaji kwa kuzingatia kuwa imesheheni wataalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter