Home VIWANDAUZALISHAJI Utafiti malikale chanzo cha mapato

Utafiti malikale chanzo cha mapato

0 comment 98 views

Utafiti wa Sayansi ya Malikale nchini umekuwa ni moja ya chanzo cha mapato Serikalini na kwa mtu mmoja mmoja.

Hii ni kutokana na makundi ya watafiti kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni kuja Tanzania kutafiti kwenye maeneo yenye urithi adhimu wa kihistoria.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Christowaja Ntandu kwenye Bonde la Olduvai ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mkoani Arusha wakati akikagua shughuli za utafiti zinazofanywa na wataalam wa ndani na wa Kimataifa wa Akiolojia.

Dkt. Ntandu amesema kuwa Tanzania inaendelea kupokea watafiti wa Akiolojia kutoka nchi mbalimbali kutafiti kwenye maeneo ya malikale yaliyopo sehemu mbalimbali nchini hususani eneo la Olduvai lenye historia kubwa ya ugunduzi wa masalia ya binadamu wa kale wanaosadikika kuishi kuanzia miaka milioni 1.7 iliyopita.

Aidha Dkt. Ntandu ameongeza kuwa watafiti hao wanapoingia nchini wanahitaji kufanya matumizi mbalimbali hususani malazi, chakula, mawasiliano, usafiri, kulipia ada ya utafiti.

Mengine ni kuwapatia ajira za muda mfupi wasaidizi wao jambo linaloingizia Taifa fedha za kigeni na kutoa ajira Kwa Watanzania.

“Watafiti hawa ni wadau wetu muhimu sana, ukiachana na matumizi yao mengine, matokeo ya tafiti zao husaidia kuvutia watalii nchini, pamoja na watafiti wengine hivyo nchini kuendelea kupata mapato.

Ndio maana nilikuja kukutana nao ili kuona na kukagua tafiti zao na kupata uwelewa wa pamoja juu ya namna nzuri ya kuendeleza tatifi hizi,” amesema Dkt. Ntandu

Akizungumzia utafiti wao, Profesa Fernando Diez Martine kutoka Chuo Kikuu Valladolid nchini Hispania, amesema wameamua kuja Tanzania kufanya utafiti kwa kuwa ni nchi yenye utajiri mkubwa wa urithi wa malikale pamoja amani na utalivu unaowafanya waweze kufanya kazi zao za kitafiti.

Ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kuhifadhi vyema maeneo ya malikale kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter