Shule za Sekondari nchini zimeshauriwa kuanzisha klabu za Historia kwa ajili ya kujenga uelewa kwa wanafunzi juu ya historia ya nchi yao na uzalendo.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Malikale nchini Dkt. Kristowaja Ntandu alipotembelea Mnara wa Kumbukumbu ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Moringe Sokoine na kukutana na uongozi wa Shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine, mkoani Morogoro.
Dkt. Ntandu ameeleza kuwa maeneo ya kihistoria ni mwalimu mzuri wa uzalendo, utu, umoja na mshikamano wa kitaifa hivyo yanapaswa kuhifadhiwa.
Naye Kaimu Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu, Hathuman Kilenja ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Malikale, kwa kuona umuhimu wa kutembelea shule hiyo kuhamasisha uhifadhi wa eneo hilo muhimu na kuanzisha klabu ya historia.