Home FEDHA Tanzania yasifiwa usimamizi mageuzi ya uchumi

Tanzania yasifiwa usimamizi mageuzi ya uchumi

0 comment 155 views

Tanzania imesifiwa kwa usimamizi mzuri na mageuzi makubwa ya kiuchumi ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hii ni katika kipindi ambacho Dunia inahangaika na misukosuko inayotokana na athari za UVIKO 19, mizozo ya vita pamoja na kuyumba kwa soko la fedha za kigeni.

Pongezi hizo zimetolewa kwa nyakati tofauti na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia (WB) anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwakwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Floribert Ngaruko, wakati wa mazungumzo na ujumbe wa Tanzania, kando ya Mikutano ya Mwaka ya WB na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Jijini Marrakech, nchini Morocco.

Wamesema kuwa mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisera na kisheria yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, yameifanya nchi kuwa na utulivu wa kiuchumi huku wakitarajia uchumi utaendelea kuimarika zaidi baada ya Serikali kufanya maboresho makubwa ya sera mbalimbali ikiwemo ya kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia sekta binafsi.

Pongezi hizo zinakuja siku moja baada ya Ripoti ya Mapitio ya Uchumi iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kubashiri kuwa kutokana na vigezo vyote vilivyotumika kupima mwenendo wa ukuaji wa uchumi katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, uchumi wa Tanzania utakua kutoka asilimia 4.7 iliyorekodiwa mwaka 2022 hadi kufikia asilimia 6.1 mwaka 2024.

Hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili kwa ukuaji wa uchumi katika nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, Viongozi hao waandamizi wa Benki ya Dunia, wamepongeza uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake kwa kusaidia fedha zitakazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa misaada ya kiufundi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano hiyo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter