Home Elimu Tanzania, Austria kushirikiana elimu ya ufundi

Tanzania, Austria kushirikiana elimu ya ufundi

0 comment 137 views

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Austria zimekubaliana kuimarisha sekta za elimu ya ufundi pamoja na utalii.

Makubaliano hayo yameafikiwa katika Mkutano wa Waziri wa Maliasili na Utalii Angelah Kairuki na Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria Prof. Martin Kocher walipokutana katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Jijini Dar es Salaam.

Waziri Kairuki amesema kuwa wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kilimo, elimu ya ufundi ambapo Tanzania kwa sasa msukumo wake ni elimu ya ufundi na tayari serikali imeanza kuboresha sera ya elimu na mitaala ya elimu.

“Austria wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika masuala ya tasnia ya ukarimu na utalii, wenzetu kwa mwaka wanapata watalii takriban milioni 40 na wamepiga hatua kubwa, nimefurahishwa pia kuona katika ujumbe alioambatana nao Prof. Kocher kuna wafanyabiashara na wawekezaji.

Na wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya utalii, uwekezaji wa hoteli na mnyororo mzima wa thamani katika sekta ya utalii,” amesema Waziri Kairuki.
Ameongeza kuwa pamoja na mambo mengine, wamekubaliana kushirikiana katika sekta za afya, pamoja na sekta binafsi nchini kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni salama na rafiki.

Naye Waziri wa Kazi na Uchumi wa Austria Prof. Martin Kocher amesema Austria itaendeleaa kushirikiana na Tanzania katika sekta mbalimbali hususan miundombinu, kilimo, usindikaji wa chakula, elimu ya ufundi, afya, ajira/kazi, nishati pamoja na utalii kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Tanzania kufungua Ubalozi wake nchini Austria, umetuwezesha kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu ya ufundi pamoja na utalii,” ameeleza Prof. Kocher.

Amebainisha kuwa asilimia 40 ya vijana nchini Austria wamekuwa wakipatiwa elimu ya ufundi katika fani mbalimbali hivyo Austria inaamini kuwa endapo watashirikiana na Tanzania kuwapatia vijana elimu ya ufundi itasaidia kuwawezesha kupata ujuzi utakaowawezesha kujenga Maisha yao na kuinua uchumi wa taifa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter