Home KILIMO Ukuaji kilimo kufika 10% ifikapo 2030

Ukuaji kilimo kufika 10% ifikapo 2030

0 comment 379 views

Serikali inaendelea na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini ikiwemo Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (5), (FYDP III) na Ajenda 10/30 ambayo inalenga kuchochea ukuaji wa kilimo kufikia asimilia 10 ifikapo mwaka 2030.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema hayo Februari 16, 2024 bungeni jijini Dodoma.

Amesema “utekelezaji wa programu hizo unaenda sambamba na Sera ya Taifa ya Kilimo (2013), Sera ya Taifa ya Umwagiliaji (2010) na Sera ya Maendeleo ya Ushirika (2002).”

Silinde alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mwantumu Dau Haji aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuendeleza kilimo nchini.

“Wizara imejiwekea mikakati ya kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula ndani ya nchi na kuuza ziada nje ya nchi, kuongeza mauzo ya mazao nje ya nchi kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 hadi Dola za Marekani Bilioni 5 ifikapo mwaka 2030, kuongeza idadi ya mashamba makubwa (block farms/commercial farms), kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023 kufikia hekta 8,500,000 sawa na ongezeko la asilimia 50 ya eneo lote linalolimwa nchini ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo cha umwagiliaji kutoka asimilia 10 hadi asimilia 50.”

Ameongeza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na nchi kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 127, kuongezeka thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo kwenda nje kutoka Bilioni 1.2 mwaka 2020 hadi Bilioni 2.3 mwaka 2023.

Aidha, ukamilishaji wa miradi ya umwagiliaji ya hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 unaendelea pamoja na kuanza miradi mipya kwa mwaka 2023/2024 yenye hekta 95,000, ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo bora ya upatikanaji wa pembejeo, kutoa ruzuku za mbolea na mbegu kwa baadhi ya mazao.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter