Home KILIMO Kiwanda kipya kumaliza tatizo la mbolea nchini

Kiwanda kipya kumaliza tatizo la mbolea nchini

0 comment 101 views

Kiwanda kipya cha mbolea cha Itracom kilichopo jijini Dodoma kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni moja za mbolea ifikapo mwezi Agosti 2024 na kuifanya Tanzania kuacha kuagiza mbolea kutoka nje.

Tani hizo milioni moja, zitakuwa ni ziada ya tani 400,000 ambapo Tanzania ina mahitaji ya mbolea tani laki sita kwa mwaka.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imefanya ziara katika kiwanda hicho ambapo kiongozi wa msafara huo Lekinyi Mollel ambae ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kiwanda hicho utasaidia nchi kujitosheleza kwa mbolea na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza pembejeo hiyo muhimu kutoka nje.

“Kuanzisha kiwanda hiki cha Itracom kunachochea fursa za kiuchumi na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea toka nje ya nchi, amesema Mollel.

Lengo la ziara hiyo ya BoT ni kujifunza mazingira ya kazi, mazingira ya uwekezaji, masuala ya masoko na mipango endelevu ya kiwanda.

“Tumefika, tumeona na tunajua kinachoendelea. Tunajifunza jinsi kiwanda kilivyojipanga kusaidia uchumi wa nchi na kuokoa uagizaji wa mbolea toka nje kwa kuzalisha hapahapa nchini,” amesema Mollel.

Awali, akizungumza na ujumbe wa Benki Kuu, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Itracom Fertilizer Ltd, Dkt. Kenneth Machuki, ameeleza kuwa “kwa sasa tuna uwezo wa kuzalisha tani laki sita (600,000), wiki ijayo tutaongeza uwezo wa kuzalisha tani 200,000 zingine na ifikapo mwezi Agosti mwaka huu tutafikia malengo yetu ya kuweza kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka”.

Kwa uzalishaji huo, Dkt. Machuki amesema Bodi ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inakadiria matumizi ya mbolea nchini kwa mwaka kuwa ni tani laki sita, hivyo kutakuwa na ziada ya tani 400,000 za kuuza nje.

Kiwanda hicho ambacho mwezekezaji anatoka nchini Burundi, ni kikubwa na cha aina yake na kinatarajiwa kuiwezesha Tanzania kutimiza lengo la kutoagiza kabisa mbolea kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2030.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter