Home KILIMO Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la njaa

Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la njaa

0 comment 288 views

Serikali itaendelea kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kutoka hekta 727,280 msimu wa 2022/2023 hadi kufikia hekta 1,200,000 ifikapo 2025.

Nyingine ni kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao zinazohimili mabadiliko ya tabianchi na usambazaji wa mbolea kwa mpango wa ruzuku ili kuweza kukabiliana na tatizo la njaa nchini.

Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde amesema hayo Bungeni jijini Dodoma Aprili 23, 2024, wakati akijibu swali la Jackson Kiswaga, Mbunge wa Kalenga kuhusu Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la njaa nchini linalotokana na upungufu wa mvua.

”Nchi yetu imekuwa ikijitosheleza kwa chakula kwa kigezo cha upimaji wa utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), kati ya asilimia 112 hadi 126 kwa kipindi cha miaka kumi (10) mfululizo.

Aidha, kutokana na mabadiliko ya tabianchi yanayoweza kusababisha upungufu wa mvua na kuhatarisha usalama wa chakula, Serikali inaendelea kuchukua hatua,” ameeleza Silinde.

Amesema katika mwaka ujao wa Fedha 2024/2025 Serikali itajenga mabwawa mapya mia moja (100) ya umwagiliaji ikiwemo katika jimbo la Kalenga ili kuweza kusaidia changamoto za mvua nyingi ambazo zimekuwa zikileta Madhara na kusaidia pale kunapokuwa na uhaba wa mvua.

Amebainisha kuwa Serikali pia itaendelea kuimarisha miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya chakula kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kutoka tani 360,000 hadi tani 500,000 ifikapo 2025.

Hadi kufikia Aprili, 2024 NFRA imenunua na kuhifadhi tani 294,069.216 kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo ambayo yatabainika kuwa na upungufu wa chakula.

Pia kutokana na mafuriko yaliyoathiri katika baadhi ya maeneo nchini katika baadhi ya maeneo Serikali kupitia kamati za Maafa za Wilaya imepewa jukumu la kutathmini kiwango cha mahitaji ya chakula na tayari Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula-NFRA wameanza zoezi hilo la ugawaji wa chakula cha msaada katika maeneo ya Rufiji, Kibiti na Mlimba.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter