Home FEDHA BoT kuja na mwongozo kutatua malalamiko ya watumiaji huduma za fedha

BoT kuja na mwongozo kutatua malalamiko ya watumiaji huduma za fedha

0 comment 7 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iko mbioni kuandaa mwongozo utakaoainisha utaratibu wa kufuatwa katika kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha.

Kaimu Mkurugenzi wa Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha Sadiki Nyanzowa, amesema mwongozo huo unalenga kuongeza ufanisi wa kushughulikia malalamiko hayo pamoja na kuleta usawa wa namna ya kushughulikia malalamiko kwa watoa huduma za fedha wote nchini.

Akizungumza na wawakilishi kutoka katika benki mbalimbali walioshiriki katika warsha ya utatuzi wa malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha nchini iliyofanyika BoT jijini Dar es Salaam Septemba 19, 2024 Nyanzowa amesema mapendekezo na maoni mbalimbali yaliyotolewa katika warsha hiyo yataisaidia BoT kutengeneza mwongozo utakaohakikisha malalamiko ya watumiaji wa huduma hizo yanashughulikiwa na kutatuliwa kwa ufanisi.

“Maoni na mapendekezo yaliyotolewa katika warsha hii yatakuwa ni sehemu muhimu katika mwongozo utakaotengenezwa na Benki Kuu ambao una lengo la kuboresha mchakato wa kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha kwa ajili ya kuongeza imani ya watumiaji wa huduma hizo,” amesema.

Aidha, ameziasa benki kuendelea kuimarisha michakato na taratibu za ndani za kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha huku zikihakikishi taratibu hizo zinaendana na miongozo mbalimbali inayotolewa na BoT.

Pia, amesema watoa huduma za fedha wanaweza kutumia malalamiko hayo kama fursa ya kuboresha huduma na bidhaa zao na hatimaye kuleta utulivu katika sekta ya fedha.

“Kwa kutazama malalamiko kuwa ni fursa ya kuboresha na kukua, badala ya kuwa ni kikwazo, watoa huduma za fedha wanaweza kupunguza vihatarishi, kujenga imani pamoja na kuleta utulivu katika sekta ya fedha kiujumla,” Nyanzowa amesema.

Nao washiriki wa warsha hiyo, wameishukuru na kuipongeza Benki Kuu kwa kupokea maoni na mapendekezo mbalimbali kutoka kwao ambayo yatatumika katika kutengeneza mwongozo wa kutatua malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter