Home FEDHA Kodi ni jambo gumu sana, si rahisi kukubalika: Rais Samia

Kodi ni jambo gumu sana, si rahisi kukubalika: Rais Samia

0 comment 223 views

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa swala la kodi ni jambo gumu sana na sio rahisi kukubalika.

Rais Samia amesema hayo Oktoba 04, 2024 wakati akizindua Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Ni ukweli kwamba kwa nyakati tofauti na kwenye vikao mbalimbali na wananchi na wadau sekta binafsi bado kumekuwa na malalamiko yanayogusa mfumo wa kodi kwa ujumla.

Malalamiko haya kuhusu ulipaji wa kodi tunaweza kuyagawa katika makundi mawili makubwa. Kundi la kwanza ni changamoto zilizopo kwa upande wa ulipaji wa kodi na pili ni changamoto zinazohusu ukusanyaji wenyewe,” ameeleza Rais.

Ameeleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanalalamikia wingi wa kodi na tozo lakini pia viwango vya kodi kutokuwa rafiki.

“Na hii ni kawaida, unajua mtu ana hiari kwenda kulipa faini bila kulazimishwa, kwa sababu faini ni kodi inayotokana na kufanya kosa, hivyo mtu akishafanya kosa akihukumiwa faini yako kiasi gani ili asiende jela mbio mbio anaenda kulipa kodi, lakini kodi hii tunayoizungumza hapa ni ya faini inayotokana na kufanya kitu kizuri.

Umefanya biashara umepata faida, una kazi yako imekutilia mapato tunakutoza faini ndio hiyo kodi yenyewe. Sasa mtu anaona nimefanya biashara nimepata fedha yangu kisha nikailipe! Nikaipe serikali bure, lakini anasahau huduma inayotolewa na serikali kwake.

Amebainisha kuwa malalamiko mengine ni swala la mifumo ya kieletroniki ya taasisi za serikali zinazotoa vibali na leseni kutosomana ni jambo linalolalmikiwa.

Mengine ni mchakato mrefu lakini pia kutozingatia weledi wakati wa ukusanyaji kodi kwa mfano matumizi ya nguvu, lugha zisizo na staha na ubabe kwa baadhi ya watumishi wa serikali.

Aidha, amebainisha kwamba kwa idadi ya Watanzania, wanalipa kodi halisi ni watu milioni mbili kati ya watu milioni sitini na tano.

“Kwa idadi yetu ya watu wanaolipa ni wachache, sasa ukitoa watoto na wengine ambao hawapaswi kukatwa kodi hatupungui labda thelathini na saba milioni, sasa hii ni ndogo sana, ina mana wanalipa watu kidogo kwa manufaa ya wengine,” ameeleza Rais.

Akizungumzia ukuaji wa uchumi wa nchi, Rais Samia amesema viashiria vyote vinaonesha kuwa uchumi unakua kwa kasi ambapo pamoja na ukuaji huo asilimia 60 ya uchumi bado upo kwenye sekta isiyo rasmi.

Ameitaka tume hiyo isaidie kutathimini, kuchambua na kutoa mapendekezo ya kuimarisha mfumo mzima wa kodi ikiwemo kwenye matumizi ya teknolojia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter