Home FEDHAMIKOPO Tunaendelea kulipa madeni: Serikali

Tunaendelea kulipa madeni: Serikali

0 comment 77 views

Serikali imesema kuwa inaendelea na utaratibu wa ulipaji wa madeni mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa chakula waliotoa huduma katika shule mbalimbali kwa kuzingatia upatikanaji wa mapato baada ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG) kufanya uhakiki wa madeni husika.

Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha Hamad H Chande wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Moshi Mjini Priscus Jacob Tarimo aliyetaka kujua mpango wa kuwalipa wazabuni wanaotoa huduma mbalimbali hususani chakula kwenye Shule za Serikali ambao wanadai kwa muda mrefu.

Chande amesema kuwa lengo la Serikali kufanya uhakiki ni kutekeleza azma ya usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma kulingana na sheria ya Bajeti Sura 439 na Sheria ya Fedha za umma Sura 348.

‘‘Wizara ya Fedha inazielekeza Halmashauri zote nchini kulipia huduma mbalimbali wanazopokea kutoka kwa watoa huduma kwa wakati ili kuepuka ulimbikizaji wa madeni na kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa watoa huduma,’’amefafanua Chande.

Kwa upande mwingine akijibu swali la Mbunge wa Chonga, Salum Mohammed Shaafi, aliyetaka kujua iwapo Akaunti ya Pamoja ya Muungano imeshafunguliwa, Chande amesema kuwa Serikali mbili zinaendelea na mashauriano juu ya mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kuhusu utaratibu wa kudumu wa Kuchangia Matumizi na Kugawana Mapato ya Muungano.

Ameongeza kuwa uamuzi wa pamoja utakapofikiwa na pande mbili za Muungano, ndiyo utakaowezesha kufunguliwa kwa Akaunti ya Fedha ya Pamoja.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter