Home BIASHARAUWEKEZAJI Uwekezaji UTT AMIS waongezeka mara mbili

Uwekezaji UTT AMIS waongezeka mara mbili

0 comment 50 views

Thamani ya mifuko ya Kampuni ya uwekezaji ya UTT AMIS imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.5354 mwezi June, 2023 hadi kufikia Shilingi trilioni 2.2382 Juni 2024.

Hili ni ongezeko la Shilingi bilioni 702.8 sawa na asilimia 45.7 ikilinganishwa na ongezeko la Shilingi bilioni 538.9 sawa na asilimia 54.0 mwaka uliopita.

Taarifa hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya UTT AMIS Prof. Faustin Rweshabura Kamuzora wakati wa mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika Novemba 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wawekezaji wakifuatilia taarifa ya uwekezaji.

Prof. Kamuzora aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo ambao ni wawekezaji katika mifuko inayosimamamiwa na kampuni hiyo ambayo ni mfuko wa Umoja, Wekeza Maisha, Watoto Fund, Jikimu, Ukwasi (Liquid) na Hati Fungani (Bond Fund) kuwa ongezeko la ukubwa wa mifuko imetokana na faida iliyopatikana katika uwekezaji pamoja na ongezeko la idadi ya wawekezaji.

“Wameongezeka wawekezaji 79,519 sawa na asilimia 32 waliojiunga katika mifuko kwa mwaka 2024 ikilinganishwa na wawekezaji 47,480 sawa na asilimia 24 waliojiunga mwaka wa fedha uliopita,” ameeleza Prof. Kamuzora huku akiongeza kuwa mifuko yote imetoa faida nzuri kwa wawekezaji wake.

Katika taarifa yake Mwenyekiti Prof. Kamuzora amebainisha kuwa katika kipindi cha mwaka ulioishia Juni 2024, kampuni iliendelea na awamu ya mwisho ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano.

Ameeleza kuwa wanatayarisha Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano ambao umejikita kuifanya kampuni kuwa mshiriki mkubwa zaidi katika soko la mitaji na dhamana nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ili kuendana na kipindi cha mipango cha Serikali, Mpango Mkakati mpya utafanyiwa mapitio ndani ya mwaka 2024/2025 ili uweze kumalizika Juni 2030.

Kati ya malengo yaliyoainishwa katika mkakati ni pamoja na kukuza thamani ya mifuko kutoka Shilingi trilioni 2.238 cha sasa hadi kufika Shilingi trilioni 7.5 na kuongeza idadi ya matawi ili kusogeza huduma kwa wawekezaji nchini na nchi za Afrika Mashariki pamoja na nchi za Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),” ameeleza Prof. Kamuzora.

Baadhi ya wawekezaji wakifuatilia taarifa ya uwekezaji.

Ameeleza kuwa katika kutekeleza hilo, UTT AMIS imekuwa ikifuatilia maendeleo ya soko katika jumuiya hizo mbili kwa kipindi cha miaka kadhaa ambapo matokeo ya awali yanaonyesha kwamba baadhi ya nchi zina fursa nzuri.

“Tutaimarisha na kuelekeza nguvu katika kuchanbua masoko haya mapya ili kufanya maamuzi sahihi na kwa wakati muafaka ukizingatia lengo la mkakati la kuongeza thamani ya mifuko ni muhimu kwa kila fursa inayopatikana iweze kutumika vyema,” ameeleza Prof. Kamuzora.

Amebainisha kuwa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa UTT AMIS ulioishia Juni 2024 umekuwa na mafanikio makubwa zaidi ya ilivyotarajiwa.

Thamani ya mifuko ilikisiwa kukua kutoka Shilingi bilioni 290.7 Juni 2019 mpaka Shilingi bilioni 485.9 kabla ya kurekebishwa na kuwa Shilingi bilioni 1,007.9 Juni 30, 2024.

“Hata hivyo thamani halisi ya mifuko mpaka kufikia Juni 2024 ilikuwa ni Shilingi trilioni 2.2 ambayo ni mara mbili ya kiwango kilichotarajiwa,” amesema.

Amesema kwa kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa mpango mpya wanatarajia kukamilisha uboreshaji wa mifumo kama msingi wa kukuza bidhaa ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma na kuibua bidhaa nyingine kwa maslahi ya wawekezaji.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter