Home FEDHA Nchi za SADC zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni

Nchi za SADC zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni

0 comment 41 views

Imeelezwa kuwa ni ukweli usiopingika kwamba nchi nyingi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni kutoka kwa Mashirika makubwa ya kifedha duniani.

Hii ni kutokana na kuongezeka kwa gharama za ukopaji katika masoko ya fedha ya kimataifa, kupungua kwa misaada na mikopo nafuu, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amesema hayo wakati akimwakilisha Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu kushiriki Mkutano wa Dharura wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Maendeleo SADC, uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom, akiwa katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha Jijini Dar es Salaam.

Katika Hotuba yake fupi, Dkt. Nchemba alieleza kuwa, ili SADC iweze kusonga mbele na kuwa na uchumi endelevu na stahimilivu, ni muhimu kutekeleza miradi ya Kimkakati ya Kikanda, kwa kutafuta rasilimali fedha kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kwa gharama nafuu ikiwemo kuutumia Mfuko wa Kikanda wa Maendeleo wa SADC utakapoanzishwa.

Alitoa wito kwa nchi wanachama kuchangia mtaji wa Mfuko wa Maendeleo wa SADC ili kuanza utekelezaji wake na kwamba Tanzania inaunga mkono pendekezo la nchi wanachama kupewa uhuru wa kuchagua njia yoyote inayoona inafaa na bora ili kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kuchangia mtaji huo.

Tanzania imepongeza na kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Jumuiya hiyo kuanzisha Mfuko wa Kikanda wa Maendeleo wa SADC.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter