Home VIWANDAUZALISHAJI Madini yenye thamani ya takribani Tsh bilioni 3.10 yapelekwa mnadani

Madini yenye thamani ya takribani Tsh bilioni 3.10 yapelekwa mnadani

0 comment 50 views

Baada ya kipindi cha miaka saba kupita, hatimae mnada wa madini ya vito umerejeshwa ambapo madini kilogramu 184.06 yenye thamani ya takribani Tsh bilioni 3.10 yaliletwa katika mnada uliofanyika Desemba 14, 2024.

Mnada huo wa madini ya vito ambao mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2017, umerejeshwa katika eneo la Mirerani mkoani Manyara.

Akizungumza katika uzinduzi wa mnada huo, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Serikali imejidhatiti kurudisha hadhi ya Tanzanite kwa kufanya minada ndani na nje ya nchi ili kuyaongezea thamani na wafanyabiashara waweze kunufaika na kuongeza pato la taifa kwa ujumla.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizindua mnada wa madini.

Waziri Mavunde amesema minada hiyo ya ndani nay a kimataifa itasaidia kuyapa thamani madini ya Tanzania.

Amesema mojawapo ya maeneo yanayosaidia kuongeza mapato ni pamoja na kudhibiti biashara ya madini, kuzuia utoroshaji na kuifanya biashara hiyo kuwa katika mfumo sahihi ambapo uwepo wa minada utachochea uongezaji thamani wa madini ya vito.

“Madini ya vito yananunuliwa kwa asilimia kubwa kwa ajili ya ‘luxury’ ni ufahari na madini ya vito tunashindana na watu wengine ndio maana Serikali inaendelea kuchukua hatua, tunarudisha hadhi ya Tanzanite ili ikashindane vizuri duniani.

Moja ya hatua ya kwanza ni urejeshaji wa minada ya ndani na ya kimataifa, ili tuyape thamani madini yetu duniani kuna madini mengi ya vito, moja ya sifa kubwa ya madini ya vito ni uadimu, Tanzanite ina sifa hizo, ila sio madini pekee yake adimu,  kuna nchi nyingine zina madini adimu ambayo hayapatikani popote hivyo tunashindana kimataifa ni lazima tuchukue hatua kuhakikisha tunarudisha hadhi ya Tanzanite katika soko la kimataifa ili na bei iweze kuongezeka na wafanyabiashara wanufaike,”amesisitiza Waziri Mavunde

Amesema, katika vipengele (category) vya  mawe duniani,  jiwe linaanzia kuwa Precious, semi-Precious halafu baadaye linakuwa jiwe la kawaida na kwamba wanachukua hatua za makusudi ili  Tanzanite lisiwe jiwe la kawaida.

“Tukiacha liwe la kawaida mtanunua kwa kilo kwa gharama ndogo sana na mtashusha hadhi ya Tanzanite, Serikali haipo tayari kuona hilo linatokea ndio maana tunayafanya haya kwa ajili ya kuhakikisha tunalinda hadhi na heshima ya jiwe letu hili, amesema Waziri Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amewahakikishia wadau wa madini kuwa Serikali haitachukua madini ya mtu baada ya mnada wa leo na kama kuna madini yatabaki yatakabidhiwa kwa wahusika.

“Kumekuwepo na hisia na dhana baada ya mnada Serikali itachukua madini yaliyobaki kwa sababu katika mnada wa mwisho wa mwaka 2017 kuna madini yalibaki na wahusika hawakurejeshewa mpaka leo, nataka niwahakikishie Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia kuhakikisha katika biashara hii pia tuwajengee ‘confidence’ mtafanya biashara kwa uhuru na hakuna namna yoyote kuwa serikali itawaingilia na kuja kuyachukua madini yenu.

“Yale madini yaliyochukuliwa yapo, yalibaki Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tumeshayatoa na tutawakabidhi rasmi wahusika ili waendelee na biashara yao ya madini, nataka niwatoe hofu na muwe na amani,” amesema Waziri Mavunde.

Waziri wa Madini Anthony Mavunde akizungumza kwenye mnada wa madini.

“Manyara tayari mna eneo ambalo tutajenga ‘Tanzanite Exchange Centre’ ambayo kwa sasa tumefanya mazungumzo na wadau tutajenga kitu kinaitwa ‘Tanzanite Smart City’ ambao utakuwa mji mkubwa wenye hoteli ndani yake, Helikopta ambazo zitatua humo humo, ukumbi mkubwa wa mikutano wahusika hivi sasa wapo Wizara ya fedha, likikamilika hili natamani siku moja mkutano mkubwa wa madini ufanyike Mirerani,” ameeleza Waziri Mavunde.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo ameongeza kuwa kupitia mnada huu idadi ya wauzaji waliojisajili kwenye mfumo wa kielektroniki wa kuendesha minada ni 195 wakiwemo wafanyabiashara wadogo wa madini (brokers) 120, wafanyabiashara wakubwa wa madini (dealers) 59, waongeza thamani madini (lapidary) 7 na wachimbaji madini 9.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda amempongeza Waziri wa Madini kwa kuweka nguvu kubwa kwenye utafiti wa madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na kuwezesha wachimbaji kuchimba bila kupoteza mitaji ikiwa ni sehemu ya “Vision 2030 ya Madini ni Maisha na Utajiri,” na kuongeza kuwa,

“Kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara lengo likiwa ni kuhakikisha mchango wa Sekta ya Madini unakua na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025”

Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka.

Naye Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amepongeza jitihada za Serikali kwa kupania kuleta mapinduzi ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa masoko na vituo vya ununuzi wa madini nchini, kuhakikisha dhahabu inanunuliwa kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivyo kuendelea kuimarisha uchumi wa nchi.

“Ninashauri Serikali kuendelea kutilia mkazo wa biashara ya madini ya vito kuendelea kufanyika katika mji wa Mirerani wakati ujenzi wa Soko la Madini Mirerani ukiendelea” amesisitiza.

Queen Sendiga, Mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Queen Sendiga ambae ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara amesema minada ya madini ya vito italeta manufaa makubwa kwa nchi ikiwa ni pamoja na kukuza kipato kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, serikali kupata mapato, kuimarisha ubora wa madini ya vito na kuongeza ushiriki wa watanzania katika Sekta ya Madini na kuwataka wananchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika sekta ya Madini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter