Home BIASHARA Biashara ya Bodaboda: Baraka au Majanga?

Biashara ya Bodaboda: Baraka au Majanga?

0 comment 183 views

Biashara ya pikipiki maarufu kama ‘bodaboda’ imekuwa moja kati ya biashara ambazo zimekuja kwa kasi sana kote nchini. Ukilinganisha na miaka kumi nyuma usafiri huu umekuja kwa kasi na kuteka soko kwa kiasi kikubwa sana. Zamani watu walitegemea usafiri wa daladala, bajaji na taxi ili kufika watakapo lakini hali imekuwa tofauti hivi sasa. Wengi wamekuwa wakikimbilia usafiri huu kwa sababu ni wa haraka na unaokoa muda kwani hutumii muda mrefu kusubiri foleni kama ilivyo kwa magari.

Tukiangazia usafiri huu kibiashara, umekuwa neema kwa watu wengi hasa vijana kwani wengi wameweza kujiajiri au kuajiriwa hivyo umepunguza tatizo la ajira kwa kiasi kikubwa sana. Hivi sasa vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha na uendeshaji bodaboda na kujiingizia kipato. Kwa upande wa wananchi, usafiri huu umerahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwani umekuwa nafuu na watanzania walio wengi wanaweza kumudu gharama zake. Pia unaokoa muda hivyo mtu anaweza kufanya shughuli nyingi zaidi na kufikisha huduma mbalimbali hata sehemu za mbali ndani ya muda mfupi.

Biashara hii pia ni uwekezaji mzuri ambao hauhitaji mtaji mkubwa sana hivyo watu wengi wanaweza wakafanya. Biashara hii inalipa kwa sababu haiangalii muda, msimu wala aina fulani ya watu katika jamii. Kila mtu ni mteja hivyo faida yake ni kubwa kama utapata dereva  muaminufu na mahesabu yako yataenda vizuri. Unaweza kuanza biashara hii na pikipiki moja na kuikuza biashara yako kutokana na faida utakayopata. Hivyo uwekezaji huu ni njia rahisi ya kujiingizia kipato endapo ukiwa makini.

Japokuwa biashara hii inakuja na neema lukuki, ina majanga yake katika jamii. Athari kubwa ambayo imezaliwa kutokana na ukuaji wa biashara ya bodaboda ni vifo au ulemavu wa kudumu. Madereva wengi wa bodaboda hawafanya mafunzo ya udereva, hawamiliki leseni, hawana uelewa wa kutosha kuhusu kanuni na sheria za barabarani na hivyo husababisha ajali nyingi hapa nchini. Wengi wamekuwa wakijiingiza katika fani hii kwa mazoea bila kufikiria kuwa wanahatarisha maisha ya watu kila wakiwa barabarani.

Pia uwepo wa biashara ya bodaboda umepelekea ongezeko kubwa la matukio ya uhalifu katika jamii. Baadhi ya madereva wa pikipiki wamekuwa sio waaminifu na wamekuwa wakishirikiana na majambazi ili kupora wananchi mali zao. Biashara hii imekuwa sio ya kuaminika kwani wengi wamekuwa wakiona madereva kama maadui zao japokuwa kuna baadhi ni waaminifu na biashara zao huathiriwa kutokana na matendo ya wenzao wachache.

Ili kufanya biashara hii kuwa endelevu na kubadilisha maisha ya wengi kiuchumi ni vizuri kama itafanywa katika utaratibu sahihi. Madereva wapate mafunzo sahihi ya kutumia vyombo vya moto na kupatiwa leseni na taasisi husika, kanuni na sheria za barabarani zifatwe na waendesha bodaboda wasiweke maisha ya abiria wao hatarini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter