Serikali imesema kuwa mashine zote za kielektoniki za kutoa risiti na kukusanya mapato maarufu kama EFD zimepata hitilafu na hazifanyi kazi kwa sasa. Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji ameeleza hayo bungeni Dodoma alipokuwa akijibu muongozo wa Spika ulioombwa na Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa.
Dk. Kijaji ameeleza kuwa tayari wataalamu wa e-government na masuala ya teknolojia (ICT) wamewasili katika ofisi za makao makuu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kubaini tatizo na kulishughulikia mara moja kwani serikali inapoteza mapato kutokana na kutokuwepo kwa mfumo huo hewani. Naye Mwenyekiti wa Bunge Mussa Zungu, ameiomba serikali kuwa makini na utatuzi wa jambo hilo kwani hitilafu hiyo inaweza kuwaletea hasara kubwa kutokana na upotevu wa mapato.