Waziri wa Fedha na Mipango Dk.Philip Mpango kuwaneemesha wafugaji na wakulima baada ya kuwasilisha bungeni mapendekezo ya kufutwa kwa kodi ya mashudu ya soya na alizeti ili kurahisisha upatikanaji wa chakula cha mifugo.
Waziri Mpango aliwasilisha mapendekezo hayo wakati akikamilisha kusoma hoja aliyoiwasilisha bungeni tarehe 14 mwezi huu wakati akiwa katika mawasilisho ya bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Waziri Mpango alisisitiza kupunguza kodi hiyo ya ongezeko la thamani (VAT) lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa chakula cha mifugo ili kuinua ufugaji hasa wa kisasa na kilimo ambavyo vimekua uti wa mgongo katika uchumi wa nchi.
Pia katika mapendekezo hayo amependekeza mabadiliko ya kuongeza kiwango cha kodi katika michezo ya bahati nasibu na mingine inayoshahibiana na hiyo lengo likiwa ni kuongeza mapato kwa serikali ambapo inakadiriwa mabadiliko hayo yataongeza makusanyo kwa Sh. 29.7 bilioni.
Hivi karibuni michezo ya kubahatisha imeshika hatamu hapa nchini ambapo watanzania wengi wamevutiwa kushiriki ili kuongeza vipato vyao.