Home VIWANDAMIUNDOMBINU Ajali za barabarani zinaturudisha nyuma

Ajali za barabarani zinaturudisha nyuma

0 comment 119 views

Kwa nchi yoyote ile, kupata maendeleo na kujijenga kiuchumi kunatokana kwa kiasi kikubwa na uwepo wa miundombinu bora ambayo inawezesha watu kwenda sehemu mbalimbali pamoja na kusafirisha mizigo yao kwa urahisi hivyo kuweka mazingira mazuri kwa ajili ya shughuli za kibiashara. Ni vigumu kuwa na maendeleo kama miundombinu hasa barabara hairidhishi. Japo barabara ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa, pia ni chanzo cha vifo vingi hapa nchini pamoja na duniani kote kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni moja  hufariki dunia kila mwaka kutokana na ajali za barabarani huku idadi kubwa ya vifo hivi ikitoka bara la Afrika. Ongezeko la vyombo vya moto katika nchi zinazoendelea inatajwa kuwa sababu kubwa ya ajali hizi. Madereva wengi wamekuwa hawazingatii kanuni na sheria za barabarani na matokeo yake taifa inapoteza nguvukazi ya taifa huku ndoto za watu wengi zikizimwa na kupotea pamoja nao.

Je ongezeko la magari hasa katika miji ni ishara ya maendeleo? Madereva wanaosababisha ajali na kuhatarisha maisha ya watu wanachukuliwa hatua za kisheria? Miundombinu yetu nayo inachangia kwa kiasi fulani katika ajali hizi? Maendeleo ya taifa nayo yanaathirika vipi kutokana namatukio ya ajali za barabarani?

Ukweli ni kwamba vijana wengi hupoteza maisha yao kutokana na ajali za barabarani. Vifo hivi mbali na kusababisha upweke na huzuni kwa familia na watu wa karibu pia inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi hawa kwa kiasi fulani. Kama aliyepoteza maisha ndio alikuwa tegemezi katika familia je maisha ya familia hiyo yanaendaje baada ya kumpoteza? Ongezeko la ajali nchini Tanzania licha ya kupunguza nguvu kazi ya taifa pia ni kikwazo kikubwa katika maendeleo. Hatua madhubuti zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa ajali za barabarani zinapungua na vifo hivi vinaepushwa. Wananchi wanalo jukumu la kufuata sheria za barabarani na kuwa makini pindi wakiwa katika vyombo vya moto.

Jamii inapaswa kujenga tabia ya kutii sheria bila shuruti ili kufanikisha lengo hili la kupunguza ajali ya barabarani. Wananchi wanao wajibu wa kutoa taarifa  za madereva wanaokiuka sheria za barabarani kwa  vyombo vya sheria. Serikali inayo inapaswa kuboresha miundombinu hii na kuhakikisha kuwa madereva wanazingatia taratibu zote zilizowekwa. Hatuweki kufikia uchumi wa kati kama nchi itaendelea kupoteza mamia ya wananchi kila mwaka kutokana na ajali za barabarani.

Ili kufikia azma iliyowekwa na serikali inapaswa kuweka mazingira salama yatakayopelekea wananchi kufanya shughuli zao za kimaendeleo bila hofu yoyote. Hivyo basi nguvu zaidi ielekezwe katika kuboresha miundombinu hapa nchini ili kuepukana na matatizo ya ajali na vifo vya barabarani.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter