Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Ephraim Kwesigabo amesema hali ya mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Juni mwaka huu umeonyesha kupungua na kufikia asilimia 3.4 ikilinganishwa na asilimia 3.6 ya mwezi Mei.
Kwesigabo amesema hayo wakati akitoa taarifa ya mfumuko wa bei wa taifa kwa mwezi Juni na kuongeza kuwa, mfumuko wa bei wa taifa hutumika kupima kasi ya mabadiliko ya bei.
Aidha, Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwezi Juni imepungua ikilinganishwa na ile ya mwezi uliopita kutokana na kupungua kwa mfumuko wa bei za baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kama bia, viyoyozi, gesi za kupikia, majiko ya mkaa pamoja na gharama za mawasiliano ambazo zimepungua kwa asilimia 2.6.
Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kwesigabo amesema kufikia mwezi Juni, mfumuko wa bei umeongezeka na kufikia asilimia 2.2 kutoka asilimia 1.7 ya mwezi Mei huku kwa nchini Kenya, mfumuko wa bei ukiongezeka na kufikia asilimia 4.28 kutoka asilimia 3.95 ya mwezi Mei.