Wadau wa zao la alizeti wamelalamikia mbegu za zao hilo zinazozalishwa nchini kuwa na ubora mdogo katika utoaji mafuta. Wamedai kuwa, uwepo wa teknolojia hafifu ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti inasababisha mengi kubaki kwenye mashudu baada ya shughuli ya uchakataji.
Zao la alizeti ni moja kati ya zao lenye kutoa faida kubwa katika kukuza uchumi wa viwanda, lakini juhudi mbalimbali za kukuza zao hilo zimekwama kutokana na teknolojia duni.
Akizungumza katika maonyesho ya kibiashara ya kimataifa, Ofisa wa taasisi ya sekta ya binafsi ya kilimo Rehema Mbunji amesema zao hilo linakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo mbegu kutokuwa na ubora. Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji wa Mafuta ya Alizeti, Ringo Ringo amesema mafuta hayo yanapendwa na mahitaji ya sasa ni tani 3000 kwa siku.
Utafiti uliofanywa na chama hicho umebaini kuwa mafuta ya kula yana soko kubwa Ulaya. Hata hivyo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Timothy Mbago amesema ni wakati wa Tanzania kuzalisha mbegu bora na kuacha kutegemea mbegu kutoka nje ya nchi.