Meneja wa kiwanda cha The Agro Processing Africa Purimui Suvuiiyu ametoa wito kwa wakulima kuacha tabia ya kuchanganya mchanga kwenye nafaka kwani kufanya hivyo kunaondoa ubora na thamani ya mazao na hivyo kuathiri soko. Sivuiiyu amesema wamegundua baadhi ya wakulima wa zao la choroko wamekuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kuongeza uzito kwenye magunia yao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja huyo amedai baadhi ya wakulima wamekuwa wakiongeza uzito kwa kuchanganya nafaka zao na mchanga hali ambayo inapelekea mazao yao kuwa na thamani ya chini. Mbali na hayo, ameongeza kuwa kiwanda hicho kinafanya biashara kimataifa hivyo kitendo cha wakulima kuchanganya zao hilo kinahatarisha ubora wake kwenye masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa Export Trading Group Fatuma Ally amesema kampuni hiyo imekuwa ikinunua mbalimbali kutoka kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuwakomboa wakulima hao na kuwasaidia kujiongezea kipato pamoja na soko japokuwa wakati mwingine choroko wanayonunua inakosa ubora unaotakiwa kwenye masoko ya nje ya nchi.